Bocco amzidi kete Kagere

Muktasari:

Washambuliaji wa Simba, Meddie Kagere, Chris Mugalu na John Bocco kila mmoja ana vitu vyake vinavyoweza kuisaidia timu hiyo, lakini Emanuel Gabriel anaweka kete yake kwa Bocco.

WASHAMBULIAJI wa Simba, Meddie Kagere, Chris Mugalu na John Bocco kila mmoja ana vitu vyake vinavyoweza kuisaidia timu hiyo, lakini Emanuel Gabriel anaweka kete yake kwa Bocco.

Wadau wengine pia wametoa mitazamo yao na baadhi ya vitu walikiri mastraika hao wanafanana kama kufunga kwa vichwa na miguu yote miwili, ingawa nje na hivyo kila mmoja ana utalamu wake.

Gabriel ambaye ni straika wa zamani wa timu hiyo,a lisema mshambuliaji ambaye anaweza akaleta madhara kwa muda wote ndani ya timu ni Bocco, alitoa sababu anaweza akacheza katikati ya mabeki wawili, lakini Kagere analikwepa eneo hilo na kukimbilia pembeni, ambako ni ngumu kukumbana na misukosuko.

“Bocco ndio maana anapata majeraha ya mara kwa mara, kwa sababu ya kucheza straika ya kati ambayo anakumbana mabeki wanaompiga sana viatu, lakini jiulize kwa nini Kagere haumii, jibu lake hawezi kufanya lolote katikati ya mabeki wawili, ndio maana fujo zake anazifanyia pembeni, hilo ndilo lililomfanya kocha akimsimamisha mmoja mbele amtumie Bocco,” alisema Gabriel na kuongeza,

“Kuhusu Mugalu bado anatakiwa aangaliwe zaidi kwenye mechi zinaoendelea, japokuwa nimemwona sio mtu wakujiuliza mara mbilimbili anapopata nafasi yaani analijua goli, hivyo katika hao watatu wote wakiwa fiti Bocco ana kila kitu chakuanza kikosi cha kwanza endapo kama atatakiwa mshambuliaji mmoja kusimama mbele,” alisema.

Staa wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogella alisema Mugalu atakuwa na kazi ya ziada mbele ya Kagere aliyeonyesha kiwango chake ndani ya misimu miwili, aliyochukua kiatu cha dhahabu, kwamba tayari anajua ligi ya Tanzania inataka nini.

Msimu wa 2018/19 Kagere alimaliza akiwa kinara wa mabao ( 23), 2019/20 (mabao 22) na msimu huu katika mechi sita, tayari ameishatupia mabao manne, jambo ambalo Mogella aliiona litampa changamoto Mugalu, kuongeza nguvu zaidi, ili kuwaaminisha Watanzania uwezo wake.

“Ujue straika mzuri ni yule anayejua kukaa kwenye nafasi yake na akaleta matokeo kwenye timu, mambo ya chenga nyingi ambazo hazina madhara sio ishu, nimeona baadhi ya vitu ambavyo wanafanana Kagere na Mugalu pamoja na Bocco, wote wanaweza wakafunga kwa vichwa, miguu ya kushoto na kulia, ila kitakachowatofautisha ni ubunifu wa mtu binafsi,” alisema. “Mugalu ameanza vizuri, lakini bado ni mapema kumfananisha na Kagere ama Bocco ambao tayari wameshafanya mengi kwenye Ligi Kuu Bara, japokuwa katika mechi alizocheza, ameweza kufunga mabao ya vichwa na kutumia miguu yote miwili kama wenzake, lakini anatakiwa kujituma zaidi ili kuingia kwenye ufalme wao,” alisema.

Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni alisema kazi kubwa ya straika ni kupeleka mipira kwenye lango la wapinzani wao, jambo aliloliona kwa wote watatu, ila anachokiona kinawatofautisha ni ubunifu.

“Bocco ana ujasiri na uzalendo wakujitolea kupambana na mabeki ndio maana amekuwa akiumia mara kwa mara, Kagere amesaka njia nyingine ya kufunga ndio maana anakimbilia pembeni na timu inapata matokeo, sasa Mugalu anatakiwa kuongeza bidii ili kocha aone umuhimu wake ndani ya kikosi cha kwanza,” alisema.

Mchambuzi wa soka, Mwalimu Alex Kashasha alisema Bocco ndiye straika hatari zaidi dhidi ya wenzake, akimchambua ana uwezo wakutafuta mipira timu inapokuwa imenyang’anywa na akaweza kufunga akipita katikati ya mabeki.

“Ni kweli Kagere ni mtaalamu sana wa kufunga akisubiria mipira katika eneo lake, tofauti na Bocco ambaye muda mwingi anawapa presha mabeki kwa kuwapita akitoka na mpira mbali, kuhusu Mugalu ni kipindi chake kuonyesha ana nini kipya cha ziada kuliko hao wenzake,” alisema.