Bocco atibua mambo Simba!

KIKOSI cha Simba leo Jumanne kitaendelea kujifua Uwanja wa Gymkhana ikiwa ni katika maandalizi ya mwisho kabla ya kucheza mechi ya mzunguko wa pili Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa kule Msimbiji, Simba ililazimisha sare ya bila mabao na sasa inajiandaa kumaliza kazi pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utapigwa Jumapili na itahitaji ushindi tu ili iweze kusonga mbele katika hatua ya makundi.

Lakini, ndani ya kambi ya Simba mambo yameanza kutia shaka na kuna dalili za kumkosa straika wao tegemeo, John Bocco ambaye msimu uliopita alifunga mabao matatu kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika ngazi ya klabu.

Bocco, ambaye ni nahodha wa Simba alitolewa kweye mchezo dhidi ya Azam FC, anaweza kukosa mchezo huo baada ya kuumia goti katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC.

Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda kwa mabao 4-2 nafasi ya Bocco ilichukuliwa na Cletous Chama ambaye alifunga bao.

Kikosi cha Simba kilifanya mazoezi Jumapili asubuhi na Bocco alikuwepo, lakini hakujiunga na wenzake.

Daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe katika kuhakikisha mchezaji huyo anapona haraka jana Jumatatu walikwenda kufanya vipimo zaidi ili kufahamu tatizo lemgo likiwa ni kuanza tiba mapema.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema hajapata taarifa rasmi kama Bocco atakosekana katika mchezo dhidi ya UD Songo.

“Kuna wachezaji wengi na kila mmoja ana umuhimu wake, lakini kukosekana kwa Bocco na wachezaji wengine ambao wanasumbuliwa na majeraha si jambo zuri kwani wangeongeza makali,” alisema.

Kwa sasa wachezaji ambao ni majeruhi mbali na Bocco ni pamoja na Ibrahim Ajibu, Wilker Da Silva na Aishi Manula aliyeumia kwenye mechi ya Taifa Stars na

Harambee Stars ya Kenya.

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Edo Kumwembe, alisema kukosekana kwa Bocco katika mchezo huo si pengo kwani kuna viungo ambao wana sifa ya kufunga kama Chama, Shiboub na hata Hassan Dilunga.

“Nafahamu Bocco ni muhimu, lakini nafasi yake wanaweza kucheza viungo wenye uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga,” alisema.