Bosi Yanga apiga mkwara

YANGA hawataki ubabaishaji na wizi kwenye mambo yao kwa sasa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla amechimba mkwara mzito akiwataka wanachama kuacha kununua jezi na vifaa vingine vya michezo vya timu hiyo ambavyo ni feki.

Ameonya kuwa kuanzia sasa ni muhimu kwa wanachama kununua jezi halisi zenye nembo ya mdhamini wao, Kampuni ya GSM.

Dk Msolla amechimba mkwara huo juzi wakati akizindua tawi la Yanga, Kata ya Kaloleni jijini hapa.

Alisema jezi za zamani ambazo zisizo na nembo ya GSM hazina manufaa kwa klabu zaidi ya kuwanufaisha wachache na kwamba, wanachama wanunue jezi halisi zenye nembo ya GSM ili kupunguza makali ya gharama za uendeshaji kwa klabu yao. “Kwanza niwapongeze Arusha kwa kuwa mstari wa mbele kuagiza jezi mpya kwa wingi, lakini kuna baadhi yenu bado wananunua jezi za zamani madukani ambazo hazina mchango kwa klabu,” alisema Dk Msolla.

Alisema kwenye uongozi wake anataka kuziba mianya yote ya matumizi ya nembo ya Yanga yasiyo na manufaa kwa klabu ikiwemo machapisho mbalimbali.

Dk Msola alisema klabu ya Yanga ina mahitaji mengi katika kugharamia wachezaji na kambi nzima, hivyo akawataka wanachama kuendelea kuchangia klabu yao.

Naye Katibu wa tawi hilo jipya, Devis Maro alisema kuna wanachama 30 halali ambapo mikakati ni kufikisha wanachama 200.

“Tunataka kufikisha idadi hiyo ili tuwe sehemu ya wanunuzi wa hisa katika klabu yetu tofauti na sasa tunachangia bila kuwa na kumbukumbu, hivyo niwatake mashabiki wote waje kujisajili kuwa wanachama halali,” alisema.

Yanga iliondokea Arusha kuelekea Afrika Kusini kukipiga na Township Rollers.