Chipukizi 5 tishio Simba, Yanga hawa

Dar es Salaam. Kiwango bora cha wachezaji chipukizi watano, wakiongozwa na beki Paul Godfrey ‘Boxer’, kimechangia kwa kiasi kikubwa kuwaweka kwenye mikono salama ndani ya klabu za Simba na Yanga.

Mbali na Godfrey, wengine ni kipa Ramadhani Kabwili, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (Yanga), Rashid Juma na Abdul Selemani waliomo katika kikosi cha Simba.

Licha ya kuzungukwa na kundi la wachezaji wenye majina makubwa na waliosajiliwa kwa fedha nyingi, chipukizi hao wamejenga imani ya benchi la ufundi kwa muda mfupi.

Tofauti na utamaduni wa Simba, Yanga kutowapa nafasi wachezaji wenye umri mdogo hasa pale zinapokabiliwa na changamoto ya ushiriki wa mashindano ya ligi na kimataifa, vijana hao wamebadili upepo ndani ya klabu hizo.

Godfrey mwenye umri wa miaka 21, amekuwa tegemeo la Yanga upande wa beki wa kulia kutokana na uwezo wake wa kudhibiti washambuliaji wa timu pinzani na kupandisha mashambulizi jambo lililomfanya amuweke benchi mkongwe Juma Abdul.

Beki huyo aliyepandishwa na Yanga kutoka timu ya vijana, anabebwa na silaha nyingine ya uvumilivu, nidhamu na kasi ndani ya uwanja na haikushangaza kuona akimudu vyema na kufanya vizuri katika mechi mbili za watani wa jadi dhidi ya Simba msimu huu.

Pia Kabwili ni hazina ya Yanga licha ya umri wake mdogo wa miaka 19 kutokana na uwezo wake wa kupanga timu na kuokoa mashambulizi ya timu pinzani.

Kipa huyo ndiye chaguo la kwanza mbele ya mwenzake Klausi Kindoki anayetokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Nyota mwingine anayetamba Yanga licha ya umri mdogo ni beki ‘Ninja’ ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa pia akitumiwa kama kiungo mkabaji.

Ubora wake wa kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani, stamina, uwezo wa kuokoa mipira ya juu na kupanga mabeki wenzake vimemfanya Ninja awe chaguo la kwanza kwa Kocha Mwinyi Zahera.

Ninja mwenye miaka 21 amesababisha mabeki wawili wazoefu, Kelvin Yondani na Andrew Vincent mmoja kati yao kuanzia benchi pindi anapoanzishwa kucheza beki wa kati.

Haishangazi kuona Zahera akikoshwa na vijana hao watatu na kuahidi kuwapa nafasi zaidi siku za usoni kutokana na kazi nzuri wanayofanya.

“Natoa nafasi kwa mchezaji anayejituma na kufanya vizuri na sidhani kama umri ni tatizo sana. Wakiendelea kufanya vizuri nitaendelea kuwapa nafasi lakini pia wapo wachezaji wengine wa kikosi chetu cha vijana nafikiria kuwapandisha,” alisema Zahera.

Kwa upande wa Juma (20) na Selemani (18) licha ya usajili wa majina makubwa ambao timu hiyo imefanya, wameweza kuwa vipenzi vya Kocha Patrick Aussems.

Juma mwenye kasi na uwezo mzuri wa kupiga chenga, msimu huu amekuwa chaguo la pili upande wa winga wa kushoto mbele ya Haruna Niyonzima aiyesajiliwa kwa Dola 60,000 (zaidi ya Sh120 milioni). Katika mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri ugenini, Juma alianzishwa kikosi cha kwanza na kung’ara.