Copa Umisseta 2018 yazidi kupamba moto

Thursday May 17 2018

 

By Imani Makongoro, Mwananchi

Dar es Salaam. Mashindano ya Shule za Sekondari (Copa Umisseta) yamezidi kushika kasi katika Kanda mbalimbali baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuyafungua rasmi juzi kwenye Kanda ya Ziwa Magharibi inayoshirikisha mikoa ya Kagera na Geita.

Uzinduzi huo ambao ulifanyika mkoani Kagera, ni mwendelezo wa mashindano hayo kwa kanda mbalimbali za nchi ambazo baadaye zitatoa washindi watakaoshiriki mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Utengenezaji Vinywaji Baridi ya Coca-Cola.

Katika uzinduzi huo Waziri Mwakyembe alivitaka vyama vya michezo kuwatumia vijana watakaoibuliwa kwenye mashindano hayo katika timu za taifa ili kupata wanamichezo wenye weledi watakaoitangaza vyema nchi.

“Mashindano hayo ndiyo msingi wa timu zetu za Taifa. Nitoe wito tu kwa vyama vya michezo nchini kuyaangalia kwa jicho la tatu,” alisema Waziri Mwakyembe.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alisema mashindano ya ngazi ya Taifa yataanza Juni 4 hadi 29.

Kiganja alisema baada ya mashindano hayo kufunguliwa rasmi kwenye Kanda ya Ziwa Magharibi, kanda inayofuata sasa ni ile ya Ziwa Mashariki ambayo mashindano yake yatafanyika kwenye Viwanja vya Chuo cha Ualimu Butimba, mkoani mwanza ambayo waandaji wake wametuma maombi maalumu ya kumuomba Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kuyafungua.

“Yataanza ya Copa Umisseta na kisha yatafuatia ya Umitashumta (kwa wanafunzi wa shule za msingi) ambayo yote yatafanyika kwenye Viwanja vya Chuo cha Butimba.”

Mashindano hayo yamewaibua nyota mbalimbali kama, Alphonce Simbu, mchezaji soka, Simon Msuva, mcheza kikapu, Hasheem Thabeet na wengineo.

Advertisement