Dakika hatari kwa Balinya hizi hapa

Herieter Makambo atakumbukwa na mashabiki wa Yanga kwa mambo mazuri aliyofanya ndani ya klabu hiyo licha ya kucheza kwa msimu mmoja tu.

Hata hivyo, mashabiki hao wanaweza kumsahau baada ya ujio wa Juma Balinya raia wa Uganda ambaye ana kiwango bora cha kufunga mabao.

Dakika 14 za mwanzo za mchezo, zinambeba Balinya na kuonekana ni mshambuliaji anayepaswa kuchungwa na mabeki.

Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, amendoka Yanga akiwa na rekodi bora ya kufunga mabao katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Makambo ambaye ni mshambuliaji halisi, alifunga mabao 17 nyuma ya Meddie Kagere (23) na Salim Aiyee aliyetua KMC akitokea Mwadui ya Shinyanga.

Wakati akisajiliwa Makambo hakuwa kipenzi cha mashabiki wake na mara kadhaa walimuona kama Yanga imekosea kumsajili katika kikosi chake.

Lakini, Makambo alithibitisha ubora uwanjani kwa kuifunga timu hiyo idadi kubwa ya mabao katika Ligi Kuu na alionekana ndiye mhimili wa Yanga.

Hata alipokosekana katika baadhi ya mechi kutokana na majeraha, Yanga iliyumba na haikupata matokeo mazuri au ilipata ushindi kwa taabu dhidi ya wapinzani wake.

Yanga sasa haitakuwa na Makambo baada ya kuuzwa katika klabu ya Horoya FC ya Guinea. Halikuwa jambo jepesi kwa mashabiki kupokea taarifa hizo, lakini ndio imeshatokea.

Kocha Mwinyi Zahera amepoza mashabiki wa Yanga kwa kumleta kinara wa mabao Juma Balinya, nyota wa zamani wa Polisi Uganda.

Ingawa kila mmoja ana aina yake ya uchezaji, lakini taratibu Balinya ameanza kuwasahaulisha mashabiki wa Yanga uwepo wa Makambo katika kikosi hicho.

Zahera alitesti mitambo yake kwa mara ya kwanza Jumapili katika mechi ya Siku ya Mwananchi ambapo Balinya alionyesha kiwango bora akicheza pacha na Sadney Urikhob raia wa Namibia.

Balinya mwenye uwezo wa kucheza namba tisa na 10 ana nafasi ya kuendeleza makali kama alivyokuwa Uganda ambapo aliibuka mfungaji bora msimu uliopita.

Zahera atakuwa na wigo mpana wa kupanga safu ya ushambuliaji, licha ya kuwanasa Balinya na Urikhob, pia inaye David Molinga aliyejiunga na klabu hiyo akitokea AC Lega ya DR Congo.

Balinya anasema anaona fahari kucheza Yanga kwa kuwa ni klabu kubwa Afrika na mkakati wake ni kuendeleza makali ya kufunga mabao msimu ujao.

“Yanga waliona kitu kwangu ndio maana waliamua kuzungumza nami, nilifurahi kwa sababu Yanga ni klabu kubwa Afrika Mashariki na wamekuwa mara kwa mara wakishiriki mashindano ya kimataifa.

“Kila mchezaji ana ndoto ya kucheza Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, niliamini naweza kutimiza ndoto hiyo nikiwa na Yanga,” anasema Balinya.

Polisi Uganda

Mshambuliaji huyo msimu uliopita alifunga mabao 19, anasema kwa muda ambao amekuwa na Yanga amejifunza mambo mapya katika soka la Tanzania.

Balinya anasema hatishwi na ushindani wa namba na amejiandaa kisaikolojia kuhakikisha anapambana kucheza kikosi cha kwanza cha Yanga.

“Napenda ushindani kwa sababu siku zote unakufanya mchezaji kuimarika, kama sehemu hakuna ushindani ni rahisi kwa mchezaji kubweteka kwa sababu hakuna mtu wa kukupa changamoto,” anasema Balinya.

Pamoja na ugeni wake Balinya anaonekana kuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kiwango alichokionyesha kwenye michezo kadhaa ya kirafiki, ikiwemo mchezo dhidi ya Mlandege ambao alipachika bao moja kwenye ushindi wa mabao 4-1.

Rekodi

Rekodi za ufungaji za Balinya zinaonyesha ni hatari kati ya dakika 31 hadi 45 kutokana na kufunga kwake msimu uliopita mabao 10 kwenye dakika hizo.

Balinya alifunga bao lake la kwanza la msimu uliopita akiwa na Polisi, Octoba 24 dhidi ya Ndejje University ambapo ilikuwa dakika ya 44 kwenye ushindi wa mabao 2-1 ambao waliupata.

Mabao mengine kati ya hayo 10, aliyoyafunga kati ya dakika 31 hadi 45, aliyafunga kwenye michezo dhidi ya Maroons, Kampala City, Express, Villa, Paidha Black na Nduparaka.

Pia Balinya ni hatari kuanzia dakika ya 76 hadi 90 kwenye dakika hizo msimu uliopita alifunga mabao manne kwenye Ligi ya Uganda ambapo ilikuwa kwenye michezo dhidi ya Paidha Black, Machi 13, Kampala, Februari, 21 zote za mwaka huu na Mbarara City, Septemba 30 mwaka jana.

Mshambuliaji huyo, alifunga mabao matatu kati ya dakika 46 hadi 75 na mawili kati ya dakika 16 hadi 30, Balinya kama asipochungwa kwenye hizo dakika zake hatari basi anaweza kuleta kizaa zaa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika idadi ya mabao 19, ambayo Balinya aliyangua msimu uliopita, aliacha gumzo Uganda kwa kufunga hat trick kwenye mchezo mmoja, ambao ulikuwa Machi 13 mwaka huu, pale ambapo Police walipoinyuka Paidha Balck kwa mabao 4-2.

Balinya anatarajia kuiongoza Yanga kwenye mchezo wa marudiano wa kuwania nafasi ya kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao watacheza tena na Township Rollers.