Fifa yaziokoa klabu za Ligi Kuu

Dar es Salaam. Agizo lililotolewa juzi na Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa), limezika rasmi hofu ya kundi kubwa la klabu za Ligi Kuu juu ya mikataba yake na wachezaji.

Idadi kubwa ya klabu zilikuwa na wasiwasi wa kuwapoteza baadhi ya wachezaji ikiwa msimu wa ligi utaendelea hadi Juni kutokana na wengi wao kuwa na mikataba inayoisha mwezi huo na kuendelea.

Kutokana na uzito wa sababu ambayo inaleta uwezekano wa msimu wa ligi kuchelewa kumalizika katika nchi nyingi duniani ambayo ni kasi ya kusambaa kwa virusi vya homa ya corona, Fifa imeamua kwamba mikataba ya wachezaji ambayo inamalizika Juni na kuendelea, ifikie tamati pale msimu kwa nchi husika utakapomalizika.

Maelekezo hayo yaliyotolewa juzi na FIFA yanaondoa uwezekano wa mchezaji kuondoka kabla msimu haujaisha jambo ambalo klabu nyingi hapa nchini zilihisi linaweza kutokea.

“Mikataba ya wachezaji inayokwisha mara nyingi imekuwa ikifikia tamati pale msimu unapomalizika. Kwa hali ya kusimama kwa mechi katika nchini nyingi, ni jambo la wazi kwamba msimu huu hauwezi kumalizika wengi kama walivyotegemea.

Hivyo inapendekezwa kwamba mikataba iendelee hadi muda ambao msimu utakuwa umemalizika. Hii inapaswa kwenda sambamba na makusudio ya pande mbili wakati wanasaini mkataba na ni lazima kuwepo na ulinzi wa uadilifu na ustahimilivu wa kimichezo,” limefafanua agizo hilo la Fifa.

Jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wilfred Kidao alizungumza na Mwananchi na kutolea ufafanuzi zaidi maelekezo hayo ya Fifa.

“Ni kweli tumeyaona na ukiyasoma maelekezo vizuri utaona wanachosisitiza ni kama msimu utaharibika,” alisema Kidao.

Klabu ambayo ilikuwa katika hatari ya kupoteza kundi kubwa la wachezaji ni Ndanda FC ambayo kwa mujibu wa katibu mkuu wake, Seleman Kachele, idadi kubwa ya wachezaji wake mikataba yao inaishia Juni.

“Kama asilimia 70 hivi ya wachezaji wetu, mikataba yao itakuwa imemalizika hivyo kabla ya kufanya mazungumzo na TFF, tutakaa chini na wachezaji wetu na kuwaelezea ili kuona kibinadamu tunafanyaje kwa sababu watakuwa na haki kwani mikataba yao haionyeshi kwamba ikitokea majanga kama haya nini kifanyike.

“Na hili ni fundisho kwa klabu na wachezaji. Ikishindikana ndipo tutajaribu kuzungumza na TFF ili kuona wanatusaidia vipi kwa sababu tunafahamu kuwa hata wao hawakupenda jambo kama hili kutokea na walipanga ligi imalizike Mei ili waweze kuendana na ratiba za mashindano ya kimataifa,” alisema Kachele.

Akizungumzia uamuzi huo wa Fifa, Mtendaji Mkuu wa KMC, Walter Harrison alisema unazipa faraja klabu.

“Ni jambo jema ukizingatia hali iliyopo sasa hakuna ambaye alitegemea iwepo na kikubwa sasa ni kuomba tatizo hili la corona limalizike mapema ili tuendelee na mashindano,” alisema Walter.

Awali, baadhi ya klabu za Ligi Kuu zilipatwa na wasiwasi wa kuondokewa na wachezaji kabla ya Ligi Kuu kuendelea tena baada ya kusimamishwa kutokana na mikataba ya baadhi yao kuishia ukingoni mwezi Juni, mwaka huu.

Wasiwasi huo ulifuatia uamuzi uliotangazwa na TFF wa kusogeza mbele muda wa ukomo wa msimu huu kutoka mwezi Mei hadi Juni 30.

Utamaduni wa idadi kubwa ya klabu za soka nchini wa kutoa mikataba mifupi ya miezi sita au mwaka mmoja kwa wachezaji, ulionekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuziweka matatani katika msimu huu ambao ligi italazimika kuchezwa kwa muda mrefu zaidi tofauti na matarajio ya wengi kutokana na janga la corona ambalo limetikisa dunia.

Ligi Kuu Bara pamoja na michezo mingine inayovutia mikusanyiko ya watu vimesimama hadi Aprili 17 ili kuwaepusha watu na maambuzi ya virusi vya corona. Hata hivyo, kusimama huko kutategemea na hali ya udhibiti wa maradhi hayo.