Hatima ya kocha Real Madrid leo

Muktasari:

  • Hatimaye baada ya presha kuanza kupungua kutokana na kufanya vizuri, klabu ya Real Madrid leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho juu ya hatima ya kocha atakayerithi mikoba ya Julen Lopetegui, nafasi kubwa anapewa kaimu kocha wa timu za vijana za klabu hiyo anayekaimu nafasi hiyo Santiago Solari.

Madrid, Hispania. Klabu ya Real Madrid leo inatarajiwa kumtangaza kocha atakayerithi mikoba iliyoachwa wazi na Julen Lopetegui.

Tangu ilipomtimua Lopetegui wiki mbili zilizopita klabu hiyo ilimteua kocha wake wa timu za vijana, Santiago Solari kukaimu nafasi hiyo na amefanya vyema kwa kushinda mechi zote alizoiongoza timu hiyo.

Bodi ya uongozi chini ya Rais wake Florentino Perez, inatarajiwa kumtangaza kocha atakayeiongoza timu hiyo kwa mkataba wa kudumu ama kumtangaza rasmi Solari kuwa kaimu kocha mkuu hadi mwisho wa msimu huu.

Solari jana aliiongoza Real Madrid kuichapa kwa mabao 4-2, Celta Vigo katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania kwa mabao ya Karim Benzema, Sergio Ramos (penalti) Dani Ceballos na bao la kujifunga la David Cabral yaliipa ushindi ulioifanya irejee katika mbio za ubingwa.

Ushindi huo umeifanya Madrid iliyoanza ligi hiyo kwa kusuasua na kusababisha kutimuliwa kwa Lopetegui kupanda hadi nafasi ya sita katika msimamo ikiwa pointi nne tu nyuma ya vinafra Barcelona ambayo jana ilipunguzwa kasi kwa kufungwa mabao 4-3 na Real Betis.

Madrid ilikuwa kwenye shinikizo kutoka kwa bodi inayosimamia Ligi Kuu Hispania kuitaka iamua kumtangaza kocha mkuu ama kumthibitisha Solari kuwa kaimu kocha hadi mwisho wa msimu.

Bodi hiyo iliipa Madrid sharti kla kutumia mapumziko ya wiki moja na nusu kupisha mechi za kimataifa za kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kufanya uamuzi juu ya hatima ya kocha mkuu kabla ya Novemba 24, ikisema baada ya hapo haitakubali benchi la ufundi liongozwe na Solari kama hajathibitishwa.

Akizungumzia kuhusu tetesi kuwa anaweza kuthibitishwa kuinoa timu hiyo hadi mwisho wa msimu huu, Solari alisema hana taarifa hizo na ikitokea basi atafurahi na kuchapa kazi kwa bidi kwani wachezaji wanamuunga mkono.

"Mimi sijali suala la kupewa timu hii moja kwa moja au kurudishwa katika timu za vijana bali ninafuraha kwamba nimefanya kazi vizuri na wachezaji, tumepata matokeo mazuri na timu imekuwa kwenye mwelekeo wa ushindani, hili ndilo ninalojivunia,” alisema Solari.

Hata hivyo kocha huyo alisema anasikitika kwamba idadi ya majeruhi katika kikosi chake inaongezeka baada ya kiungo Casemiro, beki wa kushoto Sergio Reguilon, beki wa kati Nacho Fernandez na mshambuliaji Gareth Bale kuumia.

"Unajua wachesaji wa Celta walicheza mchezo huu kama kwa kukamia wametuumizia wachezaji wetu wanne ukiiangalia faulu aliyoicheza kipa Mello kwa Gareth Bale ni wazi kuwa hawakuwa na nia nzuri kwetu,” alisema.

Mkurugenzi wa taasisi ya mahusiano ya Madrid, Emilio Butragueno, aliiambia Movistar TV kuwa kuna uwezekano mkubwa bodi ya klabu hiyo ikamthibitisha Solari.

“Nadhani kila mmoja anaona Solari alipewa jukumu zito wakati ambao kila mmoja alikata tamaa, timu ilikuwa katika wakati mgumu kutokana na matokeo mabaya lakini amefanya vizuri na sasa tunaishi kwa matumaini ya mafanikio,” alisema Butragueno