Kabunda: Nyota KMC anayeziweka mtegoni Simba, Yanga, Azam

Muktasari:

  • Ingawa Kabunda alikuwa akicheza nafasi ya beki, mwanaye Hassan ni kiungo wa pembeni ambaye ni tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Kocha Ettiene Ndairagije.

Salum Kabunda ‘Ninja’ ni jina maarufu katika medani ya soka akiwa mmoja wa mabeki shupavu wa kati waliowahi kutokea katika kikosi cha Yanga na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’.

Ninja anakumbukwa sana na mashabiki wa soka hasa Yanga kwa kuwa alikuwa kipenzi chao kutokana na uhodari wake wa kusimama vyema katika nafasi ya beki wa kati.

Libero huyo alipata umaarufu kwa kuwa alikuwa beki shupavu anayetumia nguvu muda wote na alipewa jina la utani ‘Ninja’ kutokana na uhodari wake wa kuruka kwa staili tofauti anapofuata mpira kwa adui yake.

Yanga ina beki wa kati Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye amepachikwa jina hilo na mashabiki kutokana na uhodari wake.

Ingawa Kabunda alikuwa akicheza nafasi ya beki, mwanaye Hassan ni kiungo wa pembeni ambaye ni tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Kocha Ettiene Ndairagije.

“Siwezi kukaba kwa kiwango ambacho beki anatakiwa kuwa nacho, tangu nikiwa mdogo nilipenda kufunga, nilikuwa nikicheza nafasi za mbele,” anasema Kabunda.

Simba

Kabunda anasema tangu aanze kucheza soka ya ushindani hakuwahi kucheza mechi ngumu kama ilivyokuwa dhidi ya Simba ambayo walifungwa mabao 2-1 mjini Dar es Salaam Aprili 25.

Kabunda anasema mchezo huo ulikuwa na ushindani mkali na wao waliingia uwanjani wakiwa na dhamira ya kupata pointi tatu.

“Tulianza kufungwa lakini nilifunga bao la kusawazisha. Bao nililofunga lilikuwa katika mazingira magumu, nikiwa na mpira alikuwa akinisogelea Zana kitu kama hicho,niliona kipa naye akisogea, akili ikanituma niubetue mpira, ile anatoka kipa wao akapishana nao,” anasema Kabunda.

Kabunda mwenye mabao manne katika Ligi Kuu, anasema hawakuwa na habati ya kupata ushindi katika mchezo huo kwa madai Simba ilipata penalti mbili ambazo ziliamua matokeo katika mchezo.

Yanga

Wakati ligi ikikaribia kufikia ukingoni, joto la usajili kwa klabu za Ligi Kuu limeanza kupanda na miongoni mwa wachezaji wanaowindwa ni Kabunda ambaye anahusishwa na mpango wa kujiunga na Yanga.

Kabunda ambaye huu ni msimu wa kwanza KMC aliyojiunga nayo akitokea Mwadui ya Shinyanga, anasema amefuatwa na Azam, Simba na Yanga ambazo zinataka saini yake.

“Binafsi sina tatizo juu ya kucheza Yanga au Simba kwa sababu ni timu ambazo hata kipindi kilichopita cha usajili zilikuwa zikinihitaji, siku zote nimekuwa nikitazama maslahi yangu, ndio maana ilikuwa rahisi kujiunga na KMC.

“Nina furaha hapa na najivunia kucheza KMC, lakini pia natakiwa kuangalia mbele, nilisaini mkataba wa mwaka mmoja na kikanuni naruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu yoyote pindi mkataba wangu ukiwa umebakiza miezi mitatu.

“Nimeanza kufuatwa na klabu hizo, ninachotazama ni wapi ambako watakuwa na ofa nono zaidi, nitaweka wazi wapi nitaenda endapo tukifikia pazuri katika mazungumzo hayo,” anasema Kabunda.

Azam huenda ikawa kwenye nafasi nzuri ya kumsajili winga huyo endapo kocha Ndayiragije atatua Azam kama inavyodaiwa.

Winga huyo, anasema kipa nguli na nahodha wake Juma Kaseja amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha kucheza kwa kujituma uwanjani.

Ronaldo

“Kwa kweli hapa nyumbani sipendi kusema nani namkubali kwa sababu itachukuliwa kwa mtazamo tofauti lakini Ulaya mimi ni mfuasi mkubwa wa Ronaldo, nimekuwa nikijifunza vitu vingi kwake,” anasema Kabunda.

Kabunda anasema anatamani ni kucheza timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambayo itashiriki fainali za mataifa ya Afrika, Misri fainali zilizopangwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19.

Mtoto huyo aliibukia kituo cha kukuza vipaji Dar es Salaam (DYOC) kabla ya kuchezea timu ya vijana ya Ashanti United, ambako alipandishwa hadi timu ya wakubwa na kuanzia hapo alianza kucheza Ligi Kuu.

Baada ya Ashanti kuremka daraja, mchezaji huyo ambaye mchezo wake wa kwanza Ligi Kuu ulikuwa dhidi ya JKT Ruvu, sasa JKT Tanzania akifunga bao zuri lililompatia umaarufu, alikwenda kujiunga na Mwadui ya Shinyanga ambayo aliachana nayo na kurejea Dar es Salaam.