Kagere aacha kilio kwa Jangwani

Muktasari:

Mshambuliaji wa Simba Meddie Kagere amezidi kuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani pale apatapo mpira imekuwa ni vigumu kumkabili, pambano la watani  wa jadi Yanga na Simba aliifungia timu yake bao moja lililodumu  hadi mchezo kumalizika Dk 90.

KUMDHIBITI Meddie Kagere kwa dakika 90 ni kazi sana. Waarabu wa Al Ahly wanajua hilo kwa alichowafanya Jumanne iliyopita tu! Unajua ilikuwaje? Mwarabu aliamini atapata sare kwenye Uwanja wa Taifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuona dakika zinayoyoma. Kumbe walisahau kama Kagere yumo uwanjani.

Ile paap dakika ya 64 tu akawaliza..Waarabu chali. Si ikafika jana Jumamosi, Yanga buana wamepambana wee...wakijua wametuliza mnyama, wakajisahau pia kama Kagere bado yupo uwanjani. Ghafla tu mwanangu, mara huyo kajitwisha dakika 71.

Hakuna namna Ramadhani Kabwili akaokota mpira wavuni, hadithi ikaishia hapo. Simba moja, Yanga bila. Kisha watu wakakung’uta vumbi kurudi makwao, Simba wanacheka, Yanga wamenuna.

Huenda Yanga wasiwe na hamu kabisa ya kulisikia jina la Kagere. Ndio, wana kila sababu, kwani kile alichowafanyia jana ni kama aliwatuliza kiaina baada ya zile kejeli na maneno mbofu mbofu wakati akisajiliwa Msimbazi kutoka Gor Mahia.

Wakati wa usajili mwanzoni mwa msimu, Yanga walikuwa wakimkejeli Kagere kuwa ni babu a.k.a Mhenga, lakini kwa namna alivyowanyoosha huenda hawatathubutu kumwita jina hilo tena. Straika huyo Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, aliwanyamazisha mashabiki hao wa Jangwani baada ya kufunga bao pekee na la ushindi lililoipa Simba pointi tatu muhimu katika mechi hiyo ya 102 kwa michezo ya watani wa jadi katika ligi tangu 1965.

Kagere alifunga bao hilo dakika ya 71 kwa kichwa akiwa mbele ya mabeki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Paul Godfrey pamoja na kipa Ramadhani Kabwili ambaye alishindwa kabisa kuruka kuuzuia mpira huo usitinge nyavuni.

Nahodha John Bocco, alikimbia na mpira kutoka katikati na kumimina majalo tulivu kabisa, Kagere aliruka peke yake na kuukwamisha kushoto mwa lango la Yanga na kuamsha shangwe na hoihoi zilizoanikiza kwenye Uwanja wa Taifa, uliopigwa pambano hilo la watani.

Hilo lilikuwa bao la tisa kwa Kagere katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini ni la 22 kwa mashindano yote akiichezea Simba tangu asajiliwe.

Utamu sasa ni kuwa baada ya kufunga bao hilo straika huyo asiyechoka na ambaye alipumzishwa dakika ya 90 ili kumpisha Haruna Niyonzima, aliamua kushangilia kwa kunengua.

Hata wakati wa kutoka pia alirudia tena kwa kutembea kwa mikogo na madoido yaliyomchukiza beki wa Yanga Kelvin Yondani aliyekwenda kumhimiza na kumtegea mguu naye kujiangusha, kitendo kilichomfanya mwamuzi Hans Mabena aliyelimudu pambano hilo licha ya kuwa mara yake ya kwanza kuwachezesha watani, kumpa kadi ya njano.

Lakini sasa kama hujui ni kwamba, Kagere karibu kila shindano ambalo Simba imetia mguu, amekuwa akitupia kuanzia mechi za kirafiki hadi zile za mashindano mengine na hapa chini Mwanaspoti limekuwekea mabao 22 ya straika huyo kuonyesha alivyo hatari katika kucheza na nyavu, yaani ukizubaa hakuachi buana! Huyu ndio Meddie Kagere a.k.a MK 14 kule Kenya mashabiki wa AFC Leopards wanamjua sana.