Kanda, mashine mpya Simba iliyowika TP Mazembe, Raja Casablanca

Tuesday August 20 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Deo Kanda ni jina jipya kwa mashabiki wa Simba, lakini si geni katika soka ya Afrika. Kanda amewahi kutamba kwa mabingwa wa Afrika mara tano TP Mazembe ya DR Congo kwa misimu minne. Kiungo huyo wa pembeni sasa ametua Simba huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa na maumivu ya kumkosa aliyekuwa kinara wao wa mabao wa muda wote Emmanuel Okwi alijejiunga na Al Ittihad ya Misri.

Msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, Okwi aliifanya Simba kuwa hatari katika safu ya ushambuliaji kwa kushirikiana na Meddie Kagere, John Bocco ambao alikuwa akicheza nao mara kwa mara.

Akizungumza na Spoti Mikiki, Kanda anasema kucheza kwake ligi ya mataifa tofauti ni silaha kwake ambayo inamfanya aamini anaweza kuvaa viatu vya Okwi kwa kushirikiana na akina Kagere.

“Kuziba nafasi ya mchezaji aliyefanya vizuri katika klabu kwa muda mrefu si jambo jepesi. Napaswa kufanya kazi ya ziada kwa kushirikiana na wenzake kuipa Simba mafanikio,” anasema Kanda.

“Si vibaya kubaki na kumbukumbu lakini siku zote huwa najiamini na ninauwezo wa kubadilisha mchezo, huwa najipa muda wa kuwasoma kwanza wapinzani kisha kufanya vitu ambavyo vitakuwa na faida kwa timu,” anasema Kanda.

Mshambuliaji huyo anasema amekuwa akiifahamu Simba kwa muda mrefu kutokana na ushiriki wao katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.

Advertisement

“Nimevutiwa kuja Simba kutokana na mwelekeo wa timu nilivyouona msimu uliopita, nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha tunaweka historia msimu huu,” anasema.

Ndani ya misimu miwili ambayo amecheza Simba, 2017/2018 na 2018/2019, Okwi ambaye alirejea kwenye kikosi hicho, Julai Mosi 2017 ameifungia timu hiyo mabao 36.

Okwi amekuwa ni mtu wa kutoka na kuingia Simba, awamu yake ya kwanza ilikuwa 2010 hadi 2013 ambapo alisajiliwa na timu hiyo, akitokea SC Villa ya Uganda katika miaka yake mitatu alifunga mabao 18.

Aliondoka Simba Januari 15, 2013 kwa kujiunga na Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia ambako mambo yalimuendea kombo na kuamua kurejea Uganda kwa kujiunga na SC Villa kabla ya kwenda Yanga na kutua tena Simba ambako safari hiyo, alicheza kwa mwaka mmoja 2014 hadi 2015.

Awamu ya pili Okwi kucheza Simba, aliifungia mabao 16 kwenye kipindi hicho kifupi kisha akatimkia zake SønderjyskE ya Denmark kabla ya kurejea tena Tanzania mwaka juzi na kuisaidia timu hiyo kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kanda ambaye anatazamwa kama mrithi wa Okwi, anaoenakana kuwa mzuri kwenye kutengeneza nafasi zaidi kuliko kufunga, mchezaji huyo mwenye ubunifu akiwa uwanjani mbali na kucheza TP Mazembe aliwahi pia kuitumikia Raja Casablanca ya Morocco .

Miaka ya hivi karibuni Kanda hakuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha TP Mazembe lakini alikuwa sehemu ya timu hiyo, iliyoshiriki kombe la dunia ngazi ya klabu 2010 akiwa katika ubora wake alicheza fainali ilipofungwa na Inter Milan ya Italia mabao 3-0.

Awamu ambayo Kanda alicheza kombe hilo la dunia ngazi ya klabu ni kipindi ambacho alitwaa kwa mara ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika, mara yake ya kwanza ilikuwa msimu wa 2008/09. Kama vile ambavyo Okwi alivyokuwa mtu wa kuingia na kutoka Simba basi hata upande wa Kanda nae alikuwa hivyo licha ya kuichezea TP Mazembe kwa mafanikio, 2013 alitua Raja Casablanca. Kanda alirudi DR Congo na kutua AS Vita. Alizunguka timu kadhaa na 2015 akarejea TP Mazembe kabla ya kutolewa kwa mkopo Angola ambako aliichezea 4 de Abril FC.

Advertisement