Kapombe azua jambo Stars

Thursday October 10 2019

 

By Thomas Ng’itu, Mwananchi tng’[email protected]

Dar es Salaam. Nafasi ya beki wa kulia ni moja ya maeneo yanayopaswa kuimarishwa na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ kabla ya kurudiana na Sudan Oktoba 18, mwaka huu.

Mchezo huo utakuwa wa kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan) utakaochezwa Sudan.

Kukosekana beki wa Simba, Shomari Kapombe ni pigo kwa Taifa Stars katika mchezo huo utakaochezwa Omdurman, Sudan kutokana na ubora na uzoefu wake.

Licha ya kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa na mchezo huo, Kapombe ameshindwa kuungana na wenzake jambo lililolazimisha benchi la ufundi kumuongeza beki wa KMC Boniface Maganga.

Beki huyo ameshindwa kuweka wazi sababu ya kutojiunga Taifa Stars huku akiurusha mpira kwa benchi la ufundi akidai lina taarifa zake.

Hata hivyo, chanzo cha ndani kimedai Kapombe amekacha kujiunga na Taifa Stars kwa kile anachodai kuwa na nuksi anapoitwa kuitumikia timu ya Taifa.

Advertisement

Novemba 13, 2015 Kapombe alipata majeraha ya goti wakati Taifa Stars ilipokuwa Afrika Kusini ikijiandaa kuikabili Algeria.

Julai 2017, aliumia nyonga alipokuwa mazoezi ya Taifa Stars ikijiandaa kucheza mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu Fainali za Chan dhidi ya Rwanda.

Novemba 13, 2018 alipata majeraha ya kifundo cha mguu yaliyomuweka nje muda mrefu alipokuwa kambi ya Taifa Stars Afrika Kusini ikijiandaa kuikabili Lesotho.

Kauli ya Kapombe

“Suala langu la kutojiunga na Taifa Stars watu sahihi wa kuzungumzia ni benchi la ufundi wanafahamu kila kitu,”alisema Kapombe kwa kifupi jana.

Hata hivyo, benchi la ufundi limepata kigugumizi kuzungumzia suala la Kapombe. “Kweli hayupo katika kikosi na wenzake lakini mimi si mtu sahihi wa kuzungumzia suala hilo, mimi niulize wachezaji wanaendeleaje na mazoezi na vitu vingine.

“Tanzania kuna wachezaji wengi kama Kapombe hayupo watacheza wengine katika nafasi yake na timu inaweza kufanya vizuri. Tuwaamini waliopo,”alisema kocha msaidizi wa Taifa Stars Juma Mgunda.

Kumkosa Kapombe kunaweza kuiweka Taifa Stars katika wakati mgumu dhidi ya Sudan kwa kuwa amekuwa akimudu vyema kucheza beki wa kulia kulinganisha na wazawa wengine ambao wanacheza ligi ya ndani.

Kapombe ana uwezo wa kupandisha mashambulizi na kuilinda timu kutokana na pumzi, stamina na uwezo wa kumiliki mpira na upigaji wa krosi na pasi sahihi ambazo zimekuwa zikiwafikia walengwa kwa usahihi sifa ambazo wachezaji wengine wanaocheza nafasi hizo katika ligi ya ndani hawatimizi zote.

Pia Kapombe ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi tofauti uwanjani hivyo angeweza kuwa msaada iwapo mchezaji mmoja hasa wa nafasi ya ulinzi ataumia au pale timu inapoamua kufanya mabadiliko ya kimbinu.

Kapombe ni mzoefu kutokana na idadi kubwa ya michezo ya kimataifa aliyocheza katika ngazi ya timu ya taifa na klabu.

Mchezaji ambaye anaonekana angeweza kuziba pengo la Kapombe ni nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul lakini changamoto kubwa anayokutana nayo ni kutokuwa na ufiti wa kutosha baada ya kuuguza majeraha muda mrefu.

Kukosekana Kapombe katika nafasi ya beki wa kulia, kumekuwa kukiipa wakati mgumu benchi la ufundi la Taifa Stars ambalo mara kwa mara limekuwa likilazimika kuita wachezaji tofauti ambao wanaonekana kutokuwa na ubora wa kucheza nafasi hiyo.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, wachezaji saba tofauti na Kapombe wameitwa au kupangwa kucheza nafasi hiyo ni Himid Mao, Vincent Phillipo, Salum Kimenya, Hassan Kessy, Abdallah Kheri, Paul Godfrey ‘Boxer’ na Boniface Maganga.

Advertisement