Kaze abadili gia angani

Muktasari:

Kocha wa Yanga, Cedric Kaze amesema hakuna mchezaji ambaye anaweza kuanza katika kikosi cha kwanza kwenye mechi nne mfululizo, ambazo walianza kucheza wiki iliyopita dhidi ya Polisi Tanzania hadi watakapoivaa Simba Novemba 7.

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Cedric Kaze amesema hakuna mchezaji ambaye anaweza kuanza katika kikosi cha kwanza kwenye mechi nne mfululizo, ambazo walianza kucheza wiki iliyopita dhidi ya Polisi Tanzania hadi watakapoivaa Simba Novemba 7.

Kaze alisema kwa siku 12, watacheza mechi nne na hakuna mchezaji ambaye anaweza kuanza katika michezo yote kwa muda huo mchache kwani mchezaji kama Farid Mussa hakucheza mechi ya ushindani kwa miezi saba.

“Baada ya kukaa muda mrefu bila kucheza mechi yenye ushindani juzi ndiyo alicheza dakika 60, dhidi ya Polisi alionekana kufanya vizuri na alitakiwa kupata muda wa kupumzika ikapelekea kufanya mabadiliko kwa mchezaji mwingine,” alisema Kaze na kuongezea baada ya kupata pointi sita katika michezo miwili wanapumua.

Katika mechi na KMC, miongoni mwa mabadiliko ambayo Kaze aliyafanya ni kuanza na washambuliaji Michael Surpong na Waziri Junior, ambaye alicheza kwa mara ya kwanza katika ligi msimu huu.

Kaze alisema sababu ya kuanza na mastraika wawili kwa mara ya kwanza katika mechi ya KMC kiwanja cha CCM Kirumba eneo lake la kuchezea wapinzani huwa mara nyingi wapinzani huwa wanatumia mipira mirefu.

“Baada ya kugundua hilo nikampanga Junior ambaye aina yake ya kucheza si kusimama bali alikuwa ananipa nafasi ya kucheza straika wa pili anayeweza kuzunguka eneo lote la mbele na Surpong akiwa nyuma yake, wakati mwingine anashuka mpaka kwa viungo kufuata mpira,” alisema.

“Kuanza kwao kulionekana kuwa na faida kwetu kwani Junior alifunga bao muhimu na Surpong alisababisha penalti, ambayo tulitumia kusawazisha na kiujumla wote walicheza vizuri,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kaze alisema kabla ya kuja nchini alikuwa akiifuatilia Ligi Kuu Bara na alibaini ni ngumu na mara baada ya kuanza kazi aliuona ugumu huo.