Kili Stars, Zanzibar Heroes balaa zito

Kampala, Uganda. Timu za taifa za Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, zinakabiliwa na dakika 90 za presha wakati zitakapokabiliana na Sudan na Kenya mtawalia katika mechi zao za mwisho za Kundi B la mashindano ya Chalenji yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.

Aina ya matokeo yanayohitajika kwa kila timu pamoja na takwimu zinazohusu timu hizo, zinatoa picha ya wazi ya ugumu na ushindani mkubwa ambao unaonekana utakuwepo katika mechi hiyo.

Stars ambayo inashika nafasi ya pili katika kundi B nyuma ya Kenya ikiwa na pointi tatu ilizokusanya katika michezo miwili iliyocheza dhidi ya vinara wa kundi hilo na ndugu zao wa Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ inahitajika kupata ushindi tu leo ili itinge nusu fainali.

Lakini hata ikitoka sare, inaweza kusonga mbele iwapo Zanzibar itapoteza au kutoka sare na Kenya na hata ndugu zao hao wakiibuka na ushindi, Stars inaweza kunufaika na kutinga nusu fainali ikiwa tu itamaliza ikiwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Lakini ikiwa itafungwa, Stars itaaga rasmi mashindano hayo kwani itabakia na pointi zake tatu ambazo hazitaweza kufikia zile za Kenya yenye pointi sita wala Sudan au Zanzibar ikiwa nayo itashinda mchezo wake wa mwisho.

Presha nyingine ya Stars katika mashindano hayo inaweza kuletwa na aina ya matokeo ambayo timu hizo mbilo zimekuwa zikiyapata katika mashindano ya Chalenji na mengineyo katika siku za hivi karibuni.

Zanzibar dhidi ya Kenya ni marudio ya fainali ya Chalenji 2017 ambao Kenya walishinda.