Kishindo usajili Ligi Kuu Bara

Dar es Salaam. Wakati dirisha la usajili kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara limefungwa, wadau wanasubiri kuona sura mpya kwa miamba Simba na Yanga.

Kabla ya dirisha la usajili kufungwa saa sita usiku jana, Simba ilikuwa imemnasa winga Luis Misquissone na Yanga ilimrejesha kiungo nguli Haruna Niyonzima.

Mbali na Niyonzima na Luis waliosajiliwa kwa kishindo na miamba hiyo, pia klabu nyingi zimefanya usajili zikiwemo Singida United, Azam na Polisi Tanzania.

Simba

Simba katika usajili wa dirisha dogo Simba imeachana na Mbrazili Wilker Da Silva na kumpa mkataba Luis akitokea UD Songo.

Yanga

Yanga katika dirisha hilo imewanasa Ditram Nchimbi, Yikpe Gnamien, Adeyum Saleh, Haruna Niyonzima na Tariq Seif huku ikitarajiwa kuwatoa kwa mkopo Ally Ally, Said Makapu na Rafael Daud.

Azam

Azam imemtoa kwa mkopo Paul Peter kwenda Prisons na imemsajili Never Tigere kutoka Platinumz ya Zimbabwe na Khleffin Hamdoun akitokea Mlandege Zanzibar ambao wote wanacheza nafasi ya kiungo.

Singida United

Timu hiyo ilianza ligi kwa kusuasua kabla ya kumuajiri kocha Ramadhani Nswazurwimo. Klabu hiyo imewasajili Athumani Idd ‘Chuji’, Haruna Moshi ‘Boban’, Ame Ali, Muharami Issa, Haji Mwinyi, Tumba Lui na Six Mwakasega.

Kagera Sugar

Kocha Mecky Maxime ameongeza nguvu katika kikosi chake kwa kumsajili Kelvin Sabato akitokea Gwambina. Sabato atasaidiana na mshambuliaji Yusuph Mhilu mwenye mabao sita.

Polisi Tanzania

Kuondoka kwa kocha wao msaidizi Selemani Matola na mshambuliaji wao Ditram Nchimbi ni kama imewavuruga kwani wamefanya usajili mfululizo katika dirisha dogo.

Timu hii katika dirisha hili wameanza kufanya usajili kuanzia golini baada ya kumsajili Peter Manyika huku maeneo mengine wakiwasajili Athanas Mdamu, Pius Buswita, Matheo Anthony na Jimmy Shoji.