Kiungo wa Prisons sasa njia nyeupe kutua Yanga

Dar es Salaam. Timu ya soka ya Yanga huenda ikamnasa kiungo wa Prisons, Cleoface Mkandala baada ya juhudi zake kugonga mwamba wakati wa usajili wa dirisha dogo uliopita.

Sababu iliyokuwa inatajwa Mkandala kushindwa kutua Yanga kupitia usajili wa dirisha dogo ni mkataba wake na Prisons, lakini mpaka Juni atakuwa huru.

Mchezaji huyo ameiambia Mwananchi kwamba katika usajili wa dirisha dogo alifuatwa na uongozi wa Yanga lakini alishindwa kuondoka kutokana na kubanwa na vipengele vya mkataba wake.

“Ni kweli kipindi kile Yanga ilikuwa inanihitaji. Ni mwenyekiti aliyezungumza na mimi moja kwa moja, ila mambo hayakuwa sawa,” alisema.

Alipoulizwa kama kuna timu ambazo zimepeleka maombi kuhitaji huduma yake, alijibu, “bado ni mapema kulizungumzia hilo kwa sababu Juni ndipo nitakuwa huru.

Kuhusu kutakiwa na Yanga, Azam na Gwambina FC, alisema, “huwa sipendi kuweka wazi kama mambo kabla hayajakamilika, ila mimi ni mchezaji ninayeweza kucheza popote, kikubwa ni makubaliano.

Alisema soka ni ajira na kwamba hakuna mchezaji ambaye hatamani kuitwa timu ya taifa kwa namna kocha wa timu hiyo, Ettiene Ndayiragije anavyochagua na hilo linampa moyo kwamba akifanya kazi popote ataonekana.