Kocha Mbelgiji alianzisha Yanga

Zanzibar. Zile taarifa kwamba kocha mpya wa Yanga, Luc Eymael, hataki masihara zimeanza kuonekana katika siku ya kwanza tu katika ardhi ya Tanzania baada ya Mbelgiji huyo kueleza kukerwa na upangaji wa kikosi uliochangia kung’olewa kwa timu hiyo katika nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Yanga juzi ilitolewa kwa penalti 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1. Yanga iliongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Deus Kaseke katika dakika ya 37 hadi dakika ya pili kati ya tatu za majeruhi zilioongezwa pale Mtibwa waliposawazisha kupitia kwa beki wa timu ya taifa ya U-20, Kibwana Shomari aliyemalizia kwa shuti la juu mpira wa kona fupi kutokea upande wa kulia.

Katika hatua ya kupigiana ‘matuta’, Kelvin Yondani alikosa penalti yake ya kwanza iliyogonga mwamba, lakini ilikuwa ni penalti ya kiungo Mzanzibar Abdulaziz Makame aliyejaribu kufunga kwa kuuchopu mpira kwa staili ya ‘Panenka’ na kupaisha mpira juu ya lango, iliyoonekana kumchefua kocha Luc.

Mbelgiji huyo alionekana kurusha mikono hewani kwa hasira kutokana na tukio hilo, na baada ya mechi haraka akazungumzia kutofurahishwa na benchi ya ufundi lililokuwa chini ya gwiji wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’, kuwaacha nje wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza.

Akizungumza na Mwananchi, Eymael ambaye aliushuhudia mchezo huo akiwa jukwaani alisema sio sahihi kuwadharau wapinzani.

“Huwezi kupanga kikosi kama kile katika mchezo muhimu kama ule, hii ni kama masihara, sijajua kwanini wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza hawakupewa nafasi, sio kitu kinachofurahisha,” alisema Eymael.

“Hatupaswi kuidharau timu yoyote. Tabia ya namna hii siipendi lakini pia nahitaji kufanya kazi na wachezaji wanaotambua ukubwa wa klabu hii. Kuna mambo nitaongea nao tukionana. Kwasasa hicho ndicho ninachoweza kusema.”

Kauli hiyo ya Eymael ni kama inakoleza moto uliowashwa na mashabiki wa timu hiyo walioushuhudia mchezo huo wakichukizwa na jinsi kikosi chao kilivyopangwa na hata kilivyocheza mchezo huo.

Hata hivyo, kocha msaidizi SMG ambaye ndiye aliyekuwa akiongoza Yanga katika mchezo huo alijitetea kwamba wala hawakudharau mechi hiyo kama ilivyotafsiriwa na kwamba wapo wachezaji walioomba ruhusa kwa uongozi kutokana na matatizo mbalimbali.

Maulid alisema pia wapo wachezaji wa kikosi cha kwanza waliopewa nafasi katika mechi hiyo na kwamba kutolewa kwao katika ‘matuta’ ni kama ajali.

“Angalia kipa kama Kabwili (Ramadhan) licha ya hapa anaonekana kama kipa namba tatu lakini amefanya kazi kubwa jana ameokoa penalti na kucheza vyema hii ni kama bahati mbaya kwetu kutolewa,” alisema Maulid.

“Wapo wachezaji wa kikosi cha kwanza tumewapa nafasi, tulimchezesha Balama (Mapinduzi), tulikuwa na Yondani (Kelvin), watu hawakumuona Adeyun (Saleh) ambaye krosi yake ilizalisha bao la pili katika mchezo wa Simba tulimpa nafasi jana, nafikiri tumejifunza na hawa wote ni wachezaji wa Yanga,” alisema Maulidi.

Kocha Eymael aliyezifundisha klabu mbalimbali kubwa Afrika zikiwamo AS Vita ya DRC Congo, Free State Stars na Polokwane City za Ligi Kuu ya Afrika Kusini na El Merreikh ya Sudan, anatarajiwa kusaini mkataba wa miezi 18 Yanga.