Kompany: Man City tumeweka historia mpya

Muktasari:

  • Man City imeweka historia kwa kuwa timu ya kwanza England kutwaa mataji matatu ya ndani Ligi Kuu, Kombe la Ligi na Kombe la FA. Pia ni mara ya kwanza kutwaa taji hilo tangu mwaka 1969.

Nahodha wa Manchester City, Vincent Kompany amesema timu yao ni bora zaidi duniani.

Kauli ya beki huyo wa kati imekuja muda mfupi, baada ya Man City kutwaa Kombe la FA kwa kuichapa Watford mabao 6-0 katika mechi ya fainali.

Man City imeweka historia kwa kuwa timu ya kwanza England kutwaa mataji matatu ya ndani Ligi Kuu, Kombe la Ligi na Kombe la FA. Pia ni mara ya kwanza kutwaa taji hilo tangu mwaka 1969.

“Tulianza na kujenga msingi imara wa kocha makini ambaye alijenga timu bora iliyopambana katika Ligi Kuu. Kwangu ndio timu bora duniani,” alisema Kompany.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji, alisema timu ilicheza kwa kiwango cha juu kwa miaka miwili mfululizo.

“Nilipojiunga na timu kwa mara ya kwanza hatukuwa na nafasi ya kutwaa hata kombe moja. Lakini tulianza kuondoa unyonge baada ya kuichapa Manchester United katika Kombe la FA mwaka 2011,” alisema Kompany.

Nguli huyo ameipa Man City ubingwa wa ndani mara 12 katika kipindi cha miaka minane alichocheza katika klabu hiyo.

Kompany alisema ushindi katika mechi hiyo ya nusu fainali ilikuwa ni sawa na kumfunga beki wa zamani wa Man United Rio Ferdinand.

Katika mchezo huo, Man City ilishinda bao dhidi ya Man United kabla ya kuilaza Stoke City kwenye mchezo wa fainali.

Mchezaji huyo alisema baada ya matokeo hayo, Man City ilianza kushinda mataji mbalimbali England.

Tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2008, Kompany ametwaa mataji manne ya Ligi Kuu, mawili Kombe la FA, manne Kombe la Ligi na mawili ya Ngao ya Jamii.

Mshambuliaji Raheem Sterling, aliyefunga mabao mawili kwenye Uwanja wa Wembley, alisema ndoto yao imetimia.

“Ndoto yetu imetimia. Hii ni kazi nzuri ya meneja, ametengeneza timu imara ambayo imetimiza wajibu wake,” alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa England.