Lechantre aipa Simba mtihani mgumu

Mfaransa Pierre Lechantre.

Muktasari:

Lechantre ameondoka kwa mafanikio kwa kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kukosa kwa miaka mitano. Mara ya mwisho Simba ilitwaa ubingwa mwaka 2012.

Dar es Salaam. Mfaransa Pierre Lechantre ameondoka, lakini amewaachia ujumbe mzito viongozi wa klabu ya Simba ambao utakuwa na manufaa endapo utafanyiwa kazi.

Lechantre ameondoka kwa mafanikio kwa kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kukosa kwa miaka mitano. Mara ya mwisho Simba ilitwaa ubingwa mwaka 2012.

Akizungumza Dar es Salaam jana muda mfupi kabla ya kuondoka jijini kwenda Ufaransa, kocha huyo alisema anaondoka kwa amani akiwa na rekodi nzuri Simba.

Lechantre, aliyekuwa ameingia mkataba wa miezi sita Simba, alisema kuwa ili klabu hiyo ipate mafanikio inatakiwa kujenga uwanja wa kisasa wa mazoezi na mechi.

“Simba inatakiwa kuwa na vifaa vyote vya kufanyia mazoezi, kama ‘MO’ (Mohammed Dewji) alivyosema kutakuwepo na hosteli, ‘gym’ na mambo mengine muhimu ili kupunguza gharama,” alisema Lechantre.

Hata hivyo, alisema haikuwa kazi rahisi kuinoa Simba kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza kufika Tanzania na aliwakuta wachezaji wakiwa kwenye morali ndogo.

“Niliikuta timu katika morali ya chini wachezaji wengi hawakuwa na fiti kushindana muda wote jambo ambalo nilirekebisha na timu kushindana muda wote,”aliongeza Lechantre.

Pia alidai alikuta baadhi ya wachezaji hawakuwa na nidhamu, hivyo alikemea vikali jambo hilo sanjari na kutoa adhabu ikiwemo ya kukatwa mshahara kwa mchezaji aliyekiuka utaratibu wa klabu.

Kocha huyo alimalizana na Simba Jumanne wiki hii, baada ya kukacha kukaa kwenye benchi la Simba katika mchezo wa michuano ya SportPesa ambao timu hiyo ilifungwa mabao 2-0 na Gor Mahia ya Kenya. Gor Mahia itacheza na Everton baada ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.