Leicester, Arsenal ni vita ya makocha

London, England. Wakati mashabiki wa Arsenal 30,000 watakwenda King Power, vita kubwa itakuwa kati ya makocha Unai Emery dhidi ya Brendan Rodgers.

Mashabiki hao watakwenda kuiunga mkono timu yao dhidi ya Leicester City katika mchezo wa Ligi Kuu England leo usiku.

Mbali na kutaka matokeo, pia mchezo huo utatoa majibu nani bora kati ya kocha wa Arsenal Emery na Rodgers msimu huu.

Leicester City ipo nafasi ya tatu kwa pointi 23, wakati Arsenal nafasi ya tano ikiwa na pointi zao 17, timu hizo zina tofauti ya pointi sita.

Baadhi ya mashabiki Arsenal wanamtaka Rodgers, aliyewahi kuinoa Liverpool.

Mchezo wa leo utatoa taswira halisi ya nani anayestahili kufanya kazi Emirates, Emery aliyepo kwa sasa au Rodgers anayepigiwa debe.

Leicester Ciy katika mechi nane zilizopita, imeshinda saba, imepoteza moja dhidi ya Liverpool. Zaidi ya hapo imeshinda mabao 5-0 dhidi ya Newcastle United kabla ya kuilaza Southampton 9-0.

Arsenal ina mechi nane imeshinda tatu, imefungwa moja na kutoka sare zilizobaki.

Katika mchezo uliopita Arsenal ilipocheza na Vitoria ilionyesha udhaifu mkubwa ilipopata sare ya 1-1 huku Wareno hao wakisawazisha kwa bao ambalo mfungaji alifunga mbele ya wachezaji wanane wa Arsenal waliokuwa kwenye goli lao.

Katika mechi hiyo, Arsenal ilipiga pasi sahihi 520 kati ya 579, lakini kitu cha ajabu hakuna hata pasi moja iliyopigwa ndani ya boksi la Vitoria.

Jambo hilo limewakwaza mashabiki na kufanya kelele kuwa nyingi za kumtaka aondoke ili timu apewe Rodgers. Arsenal imefunga mabao 16 tu katika mechi 11.

Kitendo cha kumshindwa kumtumia vyema Mesut Ozil, kimetajwa ni kitu kingine ambacho kitamponza Emery asipojiangalia. Matokeo ya kufungwa au sare yatamuweka matatani Emery.