Liverpool, Arsenal zakaa pazuri England

Tuesday August 20 2019

 

Liverpool imevuna pointi tatu kwa mabao ya Sadio Mane na Roberto Firmino, lakini kipa Adrian ameingia matatani baada ya kufanya kosa katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Licha ya Liverpool kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Southampton, lakini Adrian ameibua mjadala baada ya kufanya kosa lililowapa wapinzani wao bao.

Adrian alitoa pasi fyongo iliyonaswa na Danny Ings ambaye alifunga bao dakika ya 83. Siku chache zilizopita, Adrian alikuwa nyota wa Liverpool, baada ya kuokoa penalti ya kinda Tommy Abraham wa Chelsea katika mchezo wa Uefa Super Cup ambao timu hiyo ilishinda mabao 5-4 kwa penalti.

Adrian alikuwa chaguo la pili lakini aliingia kujaza nafasi ya Allison Becker ambaye ana maumivu ya kifua.

Pia katika mchezo wa jana, kipa huyo aliyesajiliwa majira ya kiangazi alianza kujaza nafasi ya Allison, lakini pamoja na kuokoa michomo mingi, kosa hilo lilimtia doa.

Inadaiwa hii si mara ya kwanza kwa Adrian kufanya kosa lililoigharimu timu katika mechi za mashindano.

Advertisement

Katika mchezo huo, beki nyota duniani, Virgil van Dijk alicheza dhidi ya timu yake ya zamani Southampton ambayo ilimuuza Liverpool kwa Pauni 75 milioni.

Dau hilo lilimfanya Dijk kuwa beki ghali duniani kabla ya Harry Maguire kumpiku baada ya kusajiliwa kwa Pauni80 milioni akitokea Leicester City majira ya kiangazi.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amemkingia kifua kipa huyo akisema ni mchezaji hodari na kosa hilo ni sehemu ya matokeo ya mchezo.

“Adrian alikuwa na maumivu ya kifundo cha mguu, alirudishiwa mipira mingi. Alipewa dawa ya kutuliza maumivu, sidhani kama bao limetokana na maumivu,” alisema Klopp.

Mechi nyingine, Arsenal iliichapa Burnley mabao 2-1, Aston Villa ililala 2-1 dhidi ya Bournemouth, Brighton na West Ham zilitoka sare bao 1-1, Everton iliichapa Watford 1-0, Norwich City iliibanjua Newcastle United 3-1 na Manchester City ilitoka sare 2-2 ilipovaana na Tottenham Hotspurs.

Advertisement