Mambo 5 yaliyoiua Simba kwa UD Songo

Dar es Salaam. Mambo matano yanaweza kuwa yamechangia Simba kutupwa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na UD Songo ya Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, juzi.

Songo imefuzu kwa kunufaika na bao la ugenini baada ya timu hizo kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Msumbiji, wiki mbili zilizopita.

Kuna sababu kadhaa zilizochangia Simba ing’oke mapema katika hatua ya awali ya mashindano hayo msimu huu ambayo msimu uliopita ilifuzu na kufika robo fainali. Eneo la kwanza ambalo liliigharimu Simba ni udhaifu wa safu za kiungo na ulinzi zilizofanya makosa ya mara kwa mara yaliyotumiwa vyema na Songo kuwazuia kupata mabao katika mchezo huo.

Viungo wa Simba walikuwa wazito kusaka mpira walipoupoteza na kujikuta wakiiweka matatani safu ya ulinzi ambayo haikucheza kwa uelewano hasa Pascal Wawa na Erasto Nyoni.

Katika kuthibitisha hilo, Kocha wa UD Songo, Chaquir Bemate alisema tangu awali alijua vyema udhaifu wa mabeki hao wa kati.

“Tuliwasoma mapema wapinzani wetu na kubaini hawana muunganiko mzuri, uzito wa mabeki wao wa kati ndio uliotusaidia,” alisema Bemate.

Jambo jingine ni kukosa ubunifu katika safu ya ushambuliaji iliyokuwa na mshambuliaji mmoja tu - asilia, Meddie Kagere aliyecheza na Chama ambaye alibadilishiwa majukumu.

Kwa muda mrefu Simba ililazimisha kushambulia kwa kutumia mipira ya krosi ambayo kwa bahati mbaya ilimkuta Kagere akiwa amezungukwa na msitu wa mabeki pasipo usaidizi.

Pia kukosekana kwa John Bocco anayecheza na Kagere mara kwa mara aliyekuwa nje akiuguza majeraha kuliikosesha Simba idadi kubwa ya mabao.

Vilevile pengo la James Kotei, Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi ni jambo jingine ambalo limechangia Simba kuondolewa mapema.

Kotei anayecheza nafasi ya kiungo wa ulinzi alikuwa silaha muhimu katika kutibua mashambulizi na mipango ya timu pinzani wakati Niyonzima alikuwa na ubunifu wa kupenya safu ya maadui na kuchezesha timu jambo ambalo juzi lilikosekana.

Kwa upande wa Okwi, ni mchezaji ambaye angeweza kusimama kama mshambuliaji wa kati na Kagere na pia angewanyima uhuru mabeki na viungo wa Songo kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho, kumiliki mpira na kufunga mabao.

Mfumo wa 4-4-2 ambao benchi la ufundi la Simba liliutumia haukuzaa matunda wala kuwa na ufanisi mbele ya Songo ambao walitumia ule wa 4-3-3 ulioifanya Simba iwe wazi eneo la katikati tofauti na wapinzani wao ambao walikuwa imara katika eneo hilo.

Jambo la mwisho ni upangaji usio sahihi wa kikosi kilichoanza na hata uamuzi wa benchi la ufundi katika kufanya mabadiliko. Pamoja na sababu hizo, Kipa Aishi Manula hakuwa fiti kwani alicheza mechi hiyo akitokea katika majeraha na juzi alianzishwa badala ya Beno Kakolanya ambaye alikuwa fiti na utayari wa mchezo.

Pia Kocha Patrick Aussems aliwaanzisha Francis Kahata na Chama ambao mechi iliyopita dhidi ya Azam FC hawakuanza huku Hassan Dilunga aliyefanya vizuri katika mechi hiyo ya Ngao ya Jamii akianzia benchi.

“Hayakuwa matarajio yetu. Mwaka uliopita tulikuwa na furaha, msimu huu tumekuwa na huzuni. Tumecheza vizuri lakini bahati haikuwa kwetu,” alisema Aussems.

Kauli za wadau

Mshambuliaji nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema Simba imefanya usajili ambao haukuwa na tija katika mashindano ya kimataifa akimtaja Kahata na wachezaji watatu raia wa Brazil, Tairone Santos da Silva, Wilker Henrique da Silva na Gerson Fraga Viera.

“Naumia sana ninapoona mchezaji anashindwa kufanya kitu ambacho nilipokuwa nacheza niliona cha kawaida, ingawa hatupaswi kulaumiana kwa kuwa soka ina matokeo ya kikatili, lakini kwa Simba hii bado,” alisema Mogella.

Nyota wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba alisema kukosekana kwa Kotei, Niyonzima na Okwi kumeigharimu timu hiyo katika mechi za kimataifa.