Mambo matatu yaitesa Yanga Ligi Kuu Bara

Dar es Salaam. Matokeo ya kupata sare katika mechi nne mfululizo iliyopata Yanga hivi karibuni yameiweka timu hiyo kwenye nafasi finyu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Katika mechi nne Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City na Polisi Tanzania kabla ya kutoka suluhu ilipovaana na Prisons, Coastal Union.

Yanga ina pointi 41 ikizidiwa 21 na Simba ambayo inaongoza kwa pointi 62 huku ikihitaji kushinda mechi tisa kati ya 14 ilizobakiwa nazo ili itangaze ubingwa.

Hata hivyo mechi tisa za Simba zinaweza kupungua endapo Yanga itaendelea kupata matokeo yasiyoridhisha katika mashindano hayo.

Wakati Yanga ikiendelea kujiuliza, mambo matatu ya ubutu wa safu ya ushambuliaji, mabadiliko ya kikosi na wachezaji kukosa pumzi ya kutosha vinaonekana kuitesa timu hiyo inayonolewa na Mbelgiji Luc Eymael.

Eymael aliyetua Yanga Januari 9 kujaza nafasi ya Mwinyi Zahera ameiongoza Yanga katika mechi 10, ameshinda nne, kapoteza mbili na sare mara nne.

Tatizo la safu ya ushambuliaji linaonekana kuitesa Yanga katika mechi hizo nne na nyingine ambazo imecheza msimu huu.

Washambuliaji David Molinga, Yikpe Gislaim,Tariq Seif, Ditram Nchimbi na Benard Morrison ndio wanaunda safu hiyo, lakini wameshindwa kuipa matokeo mazuri.

Safu hiyo imeshindwa kufua dafu katika idadi kubwa ya mechi zake licha ya viungo Mapinduzi Balama, Haruna Niyonzima na beki anayeanzisha mashambulizi Juma Abdul kutengeneza nafasi nyingi.

Hilo limethibitika katika mechi 10 ilizocheza Yanga chini ya kocha huyo imefunga mabao tisa, wastani wa bao moja kila mchezo huku Molinga akifunga matatu, Morrison, Ykpe (mawili) na Tariq bao moja.

Jambo jingine linaloitesa timu hiyo ni mabadiliko ya mara kwa mara ya kikosi chake ambapo katika mechi hizo nne, Eymael amebadili timu kwa kiasi kikubwa.

Kuanzia mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, mshambuliaji aliyecheza mechi zote tano ni Morrison na wengine wamekuwa wakifanyiwa mabadiliko mara kwa mara.

Molinga alianza dhidi ya Ruvu na Mbeya City kabla ya kumuweka benchi na kumuanzisha Yikpe ilipoikabili Prisons. Dhidi ya Polisi Tanzania alimuanzisha Tariq na juzi alimuanzisha Nchimbi kutoka winga na kumpanga mshambuliaji wa kati dhidi ya Coastal.

“Timu ina wachezaji wengi, hivyo huwezi kuwapanga wote kwa wakati mmoja, kila mechi ina aina ya wachezaji wake na mbinu fulani inategemea tunacheza na nani na wapi,”alisema Eymael.

Pia kitendo cha Yanga pumzi ya kutosha kipindi cha pili kimekuwa tatizo kwa timu hiyo kupata matokeo mazuri ingawa Eymael alisema kupata sare ni sehemu ya mchezo.

“Haya ni matokeo ya mchezo na timu yoyote inaweza kupata, muhimu ni kuangalia mechi zijazo tunapata ushindi,”alisema Eymael alipozungumzia timu yake kukosa stamina ya kutosha.

Kocha Bakari Malima alisema Yanga inapata taabu kupata ushindi kwa kuwa ilikosea katika usajili wake ambapo alidai imesajili idadi kubwa ya wachezaji wasiokuwa na msaada.