Mambo mawili kuibeba Stars

Dar es Salaam. Uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na hamasa ya mashabiki ni mambo yanayotegemewa kuibeba itakapokabiliana na Kenya Julai 28.

Taifa Stars na Kenya zitaumana katika mechi mbili nyumbani na ugenini za mtoano kuwania tiketi ya kufuzu kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (Chan).

Mchezo wa kwanza utachezwa Dar es Salaam na mechi ya marudiano itapigwa Agosti 3, Nairobi. Zikiwa zimebaki siku 10 tu za maandalizi, hakuna namna ambayo mbinu za benchi la ufundi zikawa na nafsi kubwa ya kuamua mchezo huo kwa kuwa muda ni mfupi kwa wachezaji kushika na kufanyia kazi kwa asilimia mia moja kile ambacho wataelekezwa.

Changamoto nyingine inayoilazimisha Taifa Stars kutegemea uwezo binafsi wa mchezaji mmojammoja na hamasa ya mashabiki ni mabadiliko yaliyofanyika katika benchi la ufundi baada ya kutimuliwa kwa Kocha Emmanuel Amunike na kuteuliwa Etienne Ndayiragije.

Pengine kwa kulitambua hilo, Ndayiragije alitangaza wachezaji 26 kwa ajili ya maandalizi ya mechi hizo ambao wanatoa taswira ya uteuzi huo umefanyika kwa kuangalia mahitaji ya muda mfupi na si vinginevyo.

Uteuzi wa kundi kubwa la wachezaji waliofanya vizuri katika Ligi Kuu na mashindano mbalimbali msimu uliomalizika unadhihirisha Taifa Stars inawategemea wachezaji hao kuhamishia viwango vyao katika mechi dhidi ya Kenya ili kusonga mbele.

Ibrahim Ajibu alichangia mabao 22 ya Yanga msimu uliopita akifunga sita na kupiga pasi 16 za mwisho zilizomrudisha kikosini baada ya kukosa nafasi katika Stars iliyoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), mwaka huu nchini Misri.

Lakini mwingine ni Jonas Mkude ambaye alikuwa na msimu bora ndani ya Simba na alikuwa muhimili imara katika safu ya kiungo akiiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ukiondoa wawili hao, kuna Juma Kaseja ambaye ni miongoni mwa makipa nguli waliofanya vizuri akicheza mechi 15 za Ligi Kuu na Kombe la FA bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa katika jumla ya mechi 24, na uhodari wake wa kuokoa mashambulizi ya ana kwa ana, mipira ya krosi na uzoefu alionao vinaweza kuwa chachu kwa Taifa Stars katika mashindano hayo.

Pia kuna mfungaji aliyeshika nafasi ya pili, Salim Aiyee aliyefunga mabao 18. Aiyee amesajiliwa na KMC ya Kinondoni ambayo tayari ameifungia bao moja katika Kombe la Kagame.

Ukiondoa uwezo binafsi, uamuzi wa kuwaita wanne hao wakiungana na akina Paul Godfrey ‘Boxer’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shabani Chilunda, Kelvin John na Hassan Dilunga unalenga kurudisha hamasa ya mashabiki.

Aiyee ameahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha Taifa Stars inashinda dhidi ya Kenya katika mechi zote mbili.

“Kikosi ni kizuri, tusapoti na pia tuliunge mkono benchi la ufundi kwa nguvu moja,” alisema kiungo wa zamani wa Taifa Stars, Shekhan Rashid alipozungumza na Mwananchi jana.