Mashabiki Ulaya waliombagua Sterling mbaroni

Sofia, Bulgaria. Mashabiki watano wa Bulgaria wamekamatwa kwa kosa la kuwafanyia vitendo vya ubaguzi wachezaji wa timu ya taifa ya England katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Ulaya.

Idadi kubwa ya mashabiki waliwabagua wachezaji wa England wenye asili ya Afrika wakati wa mchezo wao uliochezwa mjini Sofia, Bulgaria.

Mshambuliaji Raheem Sterling alikuwa mhanga wa tukio hilo baada ya mashabiki kumdhihaki kwa kumuita nyani.

Tukio hilo lilisababisha mchezo huo ambao England ilishinda mabao 6-0 kusimama mara mbili baada ya kocha Gareth Southgate kulalamika kwa mwamuzi.

Mashabiki watano walikamatwa na polisi baada ya kufanya uchunguzi uliowaweka matatani.

Licha ya kutolewa tangazo la kuwataka mashabiki kuacha kuwafanyia vitendo vya ubaguzi wachezaji hao, lakini walivaa fulana za rangi nyeusi zilizokuwa na ujumbe wa kutokubali maagizo hayo.

Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), limeipiga faini Bulgaria kutokana na vitendo hivyo vya ubaguzi.

Pia, shirikisho hilo linatararajia kuchukua hatua zaidi kuhusu suala hilo baada ya kujiridhisha kwa kutumia video.