Masoud yamkuta mazito Simba

Thursday September 13 2018Kocha Msaidizi wa Simba Masoud Djumaa.

Kocha Msaidizi wa Simba Masoud Djumaa. 

By THOBIAS SEBASTIAN

SIKU za kocha Msaidizi wa Simba ndani ya klabu hiyo kwa sasa zinahesabika, kwani jamaa ameachwa kwenye msafara wa timu hiyo unaondoka leo Alhamisi kwenda Mtwara kwa ajili ya mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC.

Masoud anayetajwa kuwa, kipenzi cha mashabiki wa Msimbazi ameachwa kwenye msafara huo baada ya bosi wake, Patrick Aussems kumpangia jukumu la kubaki jijini Dar es Salaam na kikosi kilichosalia ili aendelee kukinoa hadi watakaporudi.

Kikosi cha wachezaji 20 na benchi la ufundi chini ya Aussems kitaondoka asubuhi hii kwa ndege kuwahi pambano hilo litakalopigwa wikiendi hii kabla ya timu hiyo kurejea Dar tayari kwa safari ya mechi mbili za Kanda ya Ziwa.

Simba inaenda Mtwara ikiwa na kumbukumbu ya kuvuna pointi 12 ya mechi zao dhidi ya Ndanda mkoani humo, ikiwamo ushindi wa mabao 2-0 waliyowatungua ‘Wana Kuchere’ ikiwa chini ya Kocha Masoud msimu uliopita.

Jana kikosi hiki kilifanya mazoezi yao ya mwisho jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Boko Veterani ili kuteua kikosi cha wachezaji watakaoenda Mtwara na wale watakaobaki kupiga tizi sambamba na kikosi B chini ya Masoud.

Inaelezwa Masoud na kikosi kitakachosalia pamoja na timu ya vijana watakuwa wakijifua kwenye Uwanja wa WhiteSand ulio karibu na kambi ya klabu hiyo.

Mwanaspoti lilidokezwa mapema kuwa, Kocha Masoud hataambatana na timu hiyo baada ya Kocha Mkuu Mbelgiji Patrick Aussems kumtaka abaki Dar na kikosi kisichoenda Mtwara.

Kocha Aussems, alikiri kumbakisha kocha msaidizi mmoja `Dar bila kumtaja jina akidai ni utaratibu wake hata kabla hajaja Simba.

“Wachezaji watakaobaki watasalia na kocha msaidizi mmoja na huu ni utamaduni wangu na utaendelea,” alisema Aussems jana mazoezini.

Mbelgiji aliwahakikishia mabosi wake kuwa, ataenda kuifanya kazi kwa ufanisi Mtwara bila Masoud kwani atasaidiana na Kocha wa Viungo Adel Zrane na kudai uamuzi wake kumuacha Masoud ni kuhakikisha wachezaji waliobaki wanakuwa fiti.

“Hata mimi wakati nasikia maamuzi haya ya kumuacha Masoud na wachezaji watakaobaki nilishangaa, lakini alituambia tusiwe na wasi wasi kwani atasaidiana na Zrane katika mechi hiyo,” alisema mmoja wa vigogo wa Simba ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

MASOUD AFUNGUKA

Mwanaspoti ilimtafuta Kocha Masoud ambaye alikiri kwamba hataenda na timu Mtwara, lakini alisema hana tatizo na hilo kwani anaheshimu uamuzi wa bosi wake ili asimamie wachezaji waliobaki kwani wanahitaji wachezaji wote wanaocheza na wale wasiopata nafasi mara kwa mara wawe na viwango bora.

“Kuhusu kwanini siendi hilo sio swali langu, ila natambua nimeambiwa nibaki na hawa wachezaji ambao hawataenda Mtwara na tuendelee kufanya mazoezi kama kawaida, sababu nyingine nje ya hiyo mi sijui,” alisema Djuma ambaye hakutaka kuongea maneno zaidi ya hayo.

MAPROO WATUA

Katika hatua nyingine, nyota watatu wa kigeni wa Simba waliokuwa katika timu zao za taifa, Cletus Chama wa Zambia, Meddie Kagere wa Rwanda na Emmanuel Okwi aliyekuwa kwao Uganda, wametua jana kwa nyakati tofauti na wote watakwenda Mtwara.

Hata hivyo, Asante Kwasi hatoambatana na Simba kwa kuwa ana malaria na nafasi yake inazibwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Kipa chipukizi Ali Salim naye hataondoka kwani ameumia mkono.

Advertisement