Mastaa sita tishio wa kuchungwa Pyramids

Tuesday October 22 2019

 

By Charles Abel, Mwananchic [email protected]

Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika Yanga, Jumapili wiki hii wataikaribisha Pyramids ya Misri kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Mchezo huo ni wa kwanza wa hatua ya mchujo ya mashindano hayo na wiki ijayo timu hizo zitarudiana huko Cairo Misri ambapo mshindi wa jumla wa mechi mbili kati yao atatinga hatua ya makundi.

Ni mechi ngumu kwa wawakilishi hao wa Tanzania kutokana na ubora wa kikosi cha Pyramids FC ambacho kinaundwa na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika ambao wana thamani ya Euro 20 milioni (Sh 50 bilioni).

Uimara wa timu hiyo ya Misri pia unachangiwa na uwepo wa Kocha Sebastien Desabre ambaye ni raia wa Ufaransa aliyekuwa akiinoa timu ya Taifa ya Uganda kutokana na mbinu na uzoefu alionao ambao umekuwa chachu ya timu anazofundisha kufanya vizuri.

Desabre mbali na Pyramids FC na timu ya Taifa ya Uganda pia amewahi kuzinoa klabu za ASEC Mimosas, Coton Sport, Esperance, Recreativo do Libolo, JS Saoura na Ismaily.

Lakini kwa maana ya historia, Yanga inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na uzoefu wa kutosha kuzidi Pyramids kwani timu hiyo ya Misri haijawahi kupata mafanikio yoyote kwenye mashindano ya Afrika kulinganisha na wawakilishi hao wa Tanzania. Yanga imewahi kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika mara tatu ambapo moja ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998 na mara mbili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016 na mwaka 2018.

Advertisement

Katika karatasi Yanga haipewi nafasi kubwa ya kuitoa Pyramids lakini uwezekano wa hilo kutokea upo ikiwa watajiandaa vizuri kimbinu na kiufundi kwa ajili ya mechi baina ya timu hiyo.

Hata hivyo pamoja na ubora wa kikosi cha Pyramids, wapo wachezaji ambao wanaonekana kuwa tishio zaidi kwa wapinzani wa Yanga ambao bila shaka kuna ulazima wa kuwawekea ulinzi wa ziada ili wasilete madhara katika mechi hiyo na hata ile ya marudiano huko Misri.

Spoti Mikiki inakuletea orodha ya nyota sita wa Pyramids ambao wachezaji wa Yanga wanapaswa kujiandaa kikamilifu kukabiliana nao.

Ahmed El Shenawy-Kipa

Ni kipa mwenye uwezo wa hali ya juu wa kuokoa mashambulizi hasa kuchezz mipira ya krosi inayoelekezwa langoni mwake na kona lakini pia ana uwezo wa hali ya juu kusoma mchezo, kupanga safu yake ya ulinzi na pia utulivu pindi awapo langoni.

Akiwa na umri wa miaka 28, Senawy ni kipa mwenye uzoefu wa kutosha kwani amechezea klabu tofauti nchini ambazo mbali na Pyramids ni Zamalek na Al Masry na pia amekuwa miongoni mwa makipa wanaounda kikosi cha timu ya taifa ya Misri ambacho amecheza zaidi ya michezo 38.

Katika timu alizochezea ametwaa mataji matatu makubwa ambayo ni ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri aliochukua mara moja huku ubingwa wa Kombe la Chama cha Soka Misri akitwaa mara mbili.

Anatumia mguu wa kulia na kimo cha Mita 1.88

Ahmed Ayman Mansour-Beki wa Kati

Kimo chake kirefu cha Mita 1.78 na umbo lake lililojengeka vimekuwa silaha muhimu kwa beki huyo wa kati raia wa Misri mwenye umri wa miaka 25 katika kukabiliana na washambuliaji na wachezaji wa timu pinzani pindi wanapokuwa wanashambulia langoni mwake.

Ni beki anayemudu vyema kuokoa mipira ya juu, ana stamina na nguvu inayomuweza kupora mipira na kutibua mashambulizi lakini pia amekuwa akisifika kwa uwezo wake wa kurekebisha makosa yanayofanywa na wachezaji wenzake wa nafasi ya ulinzi.

Mbali na uwezo wa kucheza vyema kama beki wa kati, Mansour pia anamudu kucheza kama beki au kiungo wa upande wa kushoto.

Ragab Bakar-Beki wa kulia

Licha ya kucheza nafasi ya beki wa pembeni anapaswa kuchungwa vilivyo na wachezaji wa Yanga kwani amekuwa ni miongoni mwa nyota ambao wamekuwa chachu ya kuanzisha mashambulizi ya Pyramids FC.

Ni mchezaji mwenye kasi, stamina, pumzi na uwezo wa hali ya juu wa kumiliki mpira, kupiga pasi na krosi zinazofikia walengwa kwa usahihi lakini pia amekuwa akifanya vizuri katika kujilinda.

Na kwa kuthibitisha ni kwa namna gani alivyo muhimu, licha ya umri kuelekea kumtupa mkono akiwa na miaka 28, Bakar ni miongoni mwa wachezaji wenye thamani kubwa kikosini ambapo kwa sasa thamani yake ni Euro 400,000 (Sh 1 bilioni).

John Antwi-Mshambuliaji

Raia huyo wa Ghana ndiye chaguo la kwanza kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati wa Pyramids na ameanza katika mechi zote walizocheza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni mjanja wa kukaa kwenye nafasi sahihi pindi timu yake inaposhambulia na ana uwezo wa hali ya juu wa kufunga mabao ya vichwa lakini pia anabebwa na sifa nyingine ambazo ni uwezo wa kupiga pasi za mwisho na kumiliki mpira.

Eric Traore-Winga

Kwa asilimia kubwa mashambulizi ya Pyramids yanatengenezwa pembezoni mwa uwanja na mtu ambaye wamekuwa wakimtumia zaidi ni winga wao Eric Traore ambaye ni rais wa Burkina Faso. Kasi, chenga, uwezo wa kupiga pasi sahihi na krosi lakini pia kufunga mabao pale anapopata nafasi vimekuwa ni silaha muhimu inayotumiwa na Pyramids katika kuzimaliza timu pinzani. Ni mchezaji ambaye Yanga wanatakiwa kumdhibiti kwa nidhamu na utulivu wa hali ya juu kwani vinginevyo anaweza kuwasababishia wafanye faulo zinazoweza kuwagharimu.

Abdallah Said-Kiungo Mshambuliaji

Bila shaka Yanga wanamkumbuka vyema kiungo huyo mshambuliaji kwani ndiye aliwafanya washindwe kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2016.

Akiwa na kikosi cha Al Ahly, Said ambaye aliingia katika dakika za lala salama, alifunga bao la pili lililofanya timu yake iibuke na ushindi wa mabao 2-1 na kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam.

Ndani ya kikosi cha Pyramids kiungo huyo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 34 ndiye uti wa mgongo wa mashambulizi ya timu hiyo kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao, kuvunja safu ya kiungo na ulinzi ya timu pinzani, kuchezesha timu na kupiga pasi sahihi.

Hadi sasa nyota huyo amehusika katika mabao sita ya Pyramids msimu huu akifunga matatu na kupiga pasi tatu zilizozaa mabao katika kikosi hicho.

Advertisement