Matajiri Yanga waitwa siku ya Bob Marley

MEI 11 ya kila mwaka huwa ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha nyota wa muziki wa Reggae duniani, Bob Marley, aliyefariki mwaka 1981, lakini unaambiwa wakati mashabiki wa miondoko hiyo wakiadhimisha miaka 38 tangu gwiji huyo aiage dunia, jijini Dar kutakuwa na bonge la shughuli.

Siku hiyo ndiyo ambayo klabu ya Yanga itakuwa ikikutanisha matajiri wao kwa ajili ya kusaka mamilioni ya usajili wa kikosi chao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Ipo hivi. Yanga imedhamiria kufanya kweli kwa kusaka mabilioni ya usajili ili watishe msimu ujao na habari zikufikie tu ile kamati maalumu imewakusanya matajiri wakubwa kisha kuwafungia katika hoteli moja kukusanya fedha hizo.

Chini ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, Jangwani wamepanga kukusanya kiasi cha Sh1.5 Bilioni zitakazosaidia kufumua timu yao na kuunda upya ili wawe na kikosi cha kutisha msimu ujao na fedha hizo zimeshaanza kukusanywa huku ramani ya kupata Sh1 bilioni tu iko sawa.

Katibu wa Kamati hiyo, Deo Mutta aliliambia Mwanaspoti kamati yao imepanga ile hafla kubwa ambayo walipanga ifanyike jijini Dar es Salaam sasa itachukua nafasi Mei 11, 2019.

Alisema katika hafla hiyo ambayo itafanyika ndani ya hoteli kubwa ya Serena wamekusanya watu mbalimbali wazito na wenye ushawishi wa fedha nchini kuhudhuria kukusanya michango yao.

Alisema Mwanaspoti litakalopewa mwaliko maalum litashuhudia tukio hilo zito litakavyoweka historia na licha ya kufanyika ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan wadau wote watafuturishwa kisha baadaye pia kuwa na chakula cha usiku.

“Litakuwa ni tukio kubwa sana tunaposema timu ya wananchi na wawekezaji , tunamaanisha na siku hiyo mtaona tarehe hiyo inawezekana wenzetu Waislam watakuwa kwenye mfungo wa Ramadhan lakini tutafuturisha hapo na baadaye kuwa na chakula cha usiku.”

“Tumewapa mualiko watu wengi wenye nafasi mbalimbali pia bila kusahau wenye nguvu ya fedha pia watakuwepo ili malengo yetu yaweze kufikiwa.”

Alisema kwa sasa wanaendelea kufanya mawasiliano ya kupata mgeni rasmi katika hafla hiyo na huenda kiongozi mmoja wa nchi akaongoza harambee hiyo ambaye atatangazwa baadaye.

Ramani ya makusanyo

Katika mchoro wa kupata fedha hizo Yanga imetega vigogo wake na kuwakabidhi maeneo tofauti ambao kila mmoja amepewa kadi zake na kila kadi itakuwa na thamani ya Sh1 milioni.

Arusha

Klabu hiyo imemkabidhi aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji Samuel Lukumay kadi 50 na lengo ni kuingiza kiasi kisichopungua Sh50 milioni.

Dodoma

Akabidhiwa mwenyekiti wa kamati hiyo Mbunge wa mkoa huo mjini Antony Mavunde na amekabidhiwa kadi kuleta Sh50 milioni.

Geita

Mussa Katabaro ataongoza wenzake na amekabidhiwa kadio 15 na akitakiwa kuzirudisha na sh 15 milioni.

Wilaya ya Ilala

Amekabidhiwa kigogo Abdallah Bin Kleb na amepewa kadi 100 zitakazotakiwa kurejea na Sh100 milioni

Iringa

Madaraka Malumbo ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo amekikabidhiwa kadi 15 ambazo zitaingiza Sh15 milioni.

Kagera

Yanga imemkabidhi Pelegrinius Rutayuga ambaye alikuwa mpambe wa aliyekuwa Rais wa TFF Jamal Malinzi kuingiza Sh15 milioni akipewa kadi 15.

Katavi, Kigoma

Mkoa wa Katavi Jimmy Mafufu amekabidhiwa kadi 10 ambazo zitaingiza kiasi cha sh 10 milioni huku Mkoani Kigoma jukumu akipewa Issa Kipamba ambaye amepewa kadi kama hizo zikileta sh 10 milioni pia.

Kigamboni, Kinondoni

Hussein Ndama itakuwa chini yake akipewa jukumu la kuzinadi kadi 50 zitakazoingiza Sh50 milioni wakati Said Ntimizi akipewa kadi 100 Wilaya ya Kinondoni akitakiwa kuingiza Sh100 milioni.

Kilimanjaro, Tanga

Deo Mutta amepewa mikoa miwili kila mkoa akipewa kadi 15 na atatakiwa kuingiza Sh30 milioni.

Lindi, Mtwara

Lindi Hussein Yahaya atatakiwa kuingiza Sh10 milioni kwa kadi zake 10 huku pia akipewa 15 za Mtwara na kufanya jumla Sh25 milioni, pia Mkoa wa Manyara na Rukwa itakuwa chini ya Athuman Kihamia ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi akipewa kadi 20.

Mara, Mwanza

Amekabidhiwa jukumu mtu anaitwa Yanga Makaga ambaye huwa anaipa nguvu kubwa timu hiyo inapokwenda huko na Mwanza amepewa kadi 100 huku Mara akipewa kadi 10 akitakiwa kuingiza Sh110 milioni.

Mbeya, Njombe

Mbeya jukumu litakuwa kwa msemaji wa klabu hiyo, Dismas Tena akipewa kadi 50 zitakazoleta Sh50 milioni wakati Njombe, Debora Mkemwa amepewa kadi 10 zitakazoleta Sh10 milioni.

Pwani, Ruvuma

Pwani utakuwa chini ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo akipewa kadi 15 zikatazotakiwa kurudi na Sh15 milioni, pia Ruvuma utakuwa chini ya Mkemwa ambaye amepewa kadi 10.

Shinyanga, Singida

Mkoa wa Shinyanga utakuwa chini ya Clifford Lugora aliyepewa kadi 15 wakati Simiyu jukumu lao litakuwa chini ya Makaga tena aliyepewa kadi 10 wakati Singida wakipewa kadi 15 chini ya Mwigulu Nchemba.

Tabora, Songwe

Tabora, Said Mrisho amepewa kadi 15 wakati Songwe jukumu amepewa tena Mafufu akipewa kadi 10 na jumla wakitakiwa kuingiza Sh25 milioni.

Temeke, Ubungo

Wilaya ya Temeke itakuwa chini ya Dk David Ruhago aliyepewa kadi 100 wakati Lucas Mashauri akikabidhiwa Ubungo na kadi zake 50 na kufanya wilaya hizo kutakiwa kuleta Sh150 milioni wakati Zanzibar jukumu litakuwa kwa Abdulmalik Hassan akipewa kadi 50.

Mikoa yote hapo endapo kadi hizo zitapata wadau Yanga itakuwa na uhakika wa kuingiza Sh1 bilioni kama makusanyo hayo yataenda sawa wakati zoezi hilo likiendelea.