Matamasha yalivyobadili upepo Simba, Yanga

Tuesday August 13 2019

 

By Charles Abel, Mwananchi [email protected]

Mwanzoni mwa mwezi huu, nchi ilizizima kwa matukio matatu makubwa ya soka ambayo yalifuatana kwa ukaribu.

Agosti 4, timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ilicheza mechi ya marudiano kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (Chan), lakini pia ilikuwa ni kilele cha maadhimisho ya Tamasha la Wiki ya Mwananchi.

Siku ya Mwananchi ni tamasha la Yanga ambalo limeanzishwa mara ya kwanza likihusisha shughuli mbalimbali hasa za kijamii ambazo zilihitimishwa kwa mchezo wa kirafiki baina ya timu hiyo na Kariobang Sharks ya Kenya.

Siku mbili baadaye, yaani Agosti 6, kulikuwa na kilele cha kuadhimisha tamasha la Simba maarufu Simba Day ambapo kulichezwa mechi ya kimataifa ya kirafiki baina ya timu hiyo dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Matamasha hayo mawili ndio yalionekana kuteka hisia za wadau wa soka na Watanzania kwa ujumla hasa kutokana na shughuli ambazo zilifanyika katika kipindi cha siku kadhaa kuelekea kwenye vilele vya maadhimisho yake.

Kutokana na namna matamasha hayo mwaka huu yalivyoandika historia ya kipekee, Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya jinsi gani yanavyoweza kuwa chachu ya mabadiliko kwa klabu hizo mbili kongwe na soka la Tanzania kiujumla.

Advertisement

Kuongeza mtaji wa mashabiki

Shabiki ni mdau muhimu sana katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu mahala popote pale duniani na uwepo wake una faida kubwa katika mchezo huo wa soka.

Matamasha ya Simba Day na Siku ya Mwananchi yanaweza kuwa fursa nzuri na ya kipekee kwa klabu za Yanga na Simba kuongeza idadi ya mashabiki wake na kuwawelinda wale waliopo kwa sasa.

Matukio mbalimbali yanayoambatana na matamasha hayo kama vile ufanyaji wa usafi kwenye mitaa na taasisi mbalimbali, kuchangia damu, kusaidia wasiojiweza na watoto yatima alikadhalika wagonjwa mahospitalini, yanaweza kujenga ushawishi na mvuto kwa kundi kubwa la watu kutamani au kujiona nao ni sehemu ya klabu.

Lakini pia matamasha haya yanafungua milango kwa kizazi kipya kuzipenda na kuwa mashabiki waaminifu na wenye mapenzi na timu hizo siku za usoni.

Kuongezeka kwa namba ya mashabiki kuna faida ya kuvutia wadhamini na kufungua fursa nyingine za kiuchumi kwa klabu hizo.

Fursa kibiashara/kiuchumi

Tumeshuhudia kampuni ya ubashiri wa matukio ya michezo ya SportPesa mwaka huu ikidhamini tamasha la Simba Day ambalo lilikuwa likitimiza miaka 10.

Maana yake Simba imevuna kiasi kikubwa cha fedha kutoka SportPesa ambao walikuwa ni wadhamini wakuu wa tukio hilo mwaka huu.

Kwa upande wa Yanga tumeshuhudia pia kampuni za GSM na Taifa Gas nazo zikidhamini Tamasha lao la Siku ya Mwananchi.

Fedha hizo zisingepatikana kama klabu hizo zisingekuwa na matamasha ya namna hiyo ambayo yamekutanisha umati mkubwa wa mashabiki wa timu hizo mbili kongwe.

Lakini ukiondoa fedha za udhamini, klabu hizo zimeweza kuuza jezi na bidhaa nyingine kupitia matamasha hayo, zimeingiza fedha kutokana na viingilio vya mashabiki kwenye mechi zilizocheza siku ya kilele cha matamasha hayo lakini pia watu binafsi wameingiza kipato kutokana na biashara mbalimbali walizozifanya wakati wa matamasha hayo.

Mapato hayo yaliyopatikana yatasaidia klabu zetu kujiendesha lakini pia kuboresha maisha ya mtu mmojammoja.

Kuimarisha umoja na mshikamano

Ni matamasha ambayo yanakutanisha pamoja kundi kubwa la wapenzi na mashabiki wa timu hizo panoja na wadau wa soka nchini ambao aghalabu hupata nafasi finyu ya kujumuika pamoja pindi msimu utakapokuwa ukiendelea.

Lakini pia ni sehemu ya watu kujifunza mila, desturi na utamaduni wa klabu hizo mbili kongwe nchini.

Hili lina faida ya kulinda historia ya Simba na Yanga ambayo imekuwa ikidumu kizazi hadi kizazi na kutoiweka kwenye hatari ya kutoweka

Kuwajenga wachezaji kisaikolojia

Ni matukio yanayompa deni mchezaji na kumuongezea molali kuelekea msimu mpya wa mashindano.

Matamasha hayo ni wazi kwamba humfanya mchezaji kutambua jukumu na wajibu mkubwa alionao kuhakikisha anaipatia klabu mafanikio katika msimu unaofuata.

Advertisement