Matokeo ya kushangaza kufuzu Afcon 2021

Kipenga cha mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 yatakazofanyika nchini Cameroon, kilipulizwa rasmi kuanzia Alhamisi wiki iliyopita.

Jumla ya timu za mataifa 48 zilizogawanywa katika makundi 12 zinasaka nafasi 23 za kushiriki awamu inayofuata ya fainali za Afcon baada ya zile za mwaka huu zilizofanyika nchini Misri ambako Algeria ilitwaa ubingwa.

Katika kipindi hiki cha kalenda ya kimataifa ya mashindano, kila timu iliyopo katika hatua ya makundi ya mashindano hayo itacheza mechi mbili na baada ya hapo, mechi zingine zitachezwa mwakani katika miezi ya Agosti, Septemba, Oktoba na Novemba.

Baada ya kucheza na Guinea ya Ikweta Ijumaa iliyopita, timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kesho Jumanne itakuwa kibaruani kuikabili Libya ugenini nchini Tunisia ikiwa ni mojawapo ya michezo ya kundi J wakati mechi nyingine ya kundi hilo itakuwa ni baina ya Guinea ya Ikweta itakayocheza na Tunisia ikiwa nyumbani. Katika mechi za ufunguzi wa pazia la mashindano ya kuwania kufuzu kumekuwapo na matokeo tofauti kwa timu 48 zinazoshiriki mashindano hayo ambapo zipo zilizopata matokeo mazuri ikiwemo Stars iliyoshinda 2-1, sare na kuna ambazo zimepoteza.

Katika hali ya kushangaza, zipo baadhi ya mechi ambazo zilikuwa na matokeo yaliyostaajabisha wengi kwa baadhi ya timu zinazoonekana tishio kushindwa kupata ushindi, na pia ushindi kwa timu kadhaa ambazo zinatazamwa kama ndogo au za kiwango cha wastani.

Spoti Mikiki inakuletea orodha ya matokeo ya kushangaza kwa mechi za raundi ya kwanza ya kuwania kufuzu Fainali za Afcon 2021 ambayo kwa namna moja au nyingine hayakutegemewa na wengi kutokea.

Togo 0-1 Comoro

Visiwa vya Comoro vimekuwa vikionekana kama moja ya nchi zenye viwango duni vya soka barani Afrika na ni vigumu kuipa nafasi ya kupata ushindi pindi inapocheza ugenini dhidi ya timu zenye wachezaji wa daraja la juu, na ambazo zinafanya vyema katika soka hapa Afrika.

Hata hivyo, Alhamisi ilileta mshtuko baada ya kuichapa Togo ugenini kwa bao 1-0 ushindi ulioifanya ikamate uongozi wa kundi G ambalo pia lina timu za Kenya na Misri.

Ushindi huo ulikuwa ni dhidi ya Togo iliyojaza idadi kubwa ya nyota wanaotamba katika klabu mbalimbali duniani kama vile nyota wa zamani wa Arsenal, Gilles Sunu na mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2018/2019, Kodjo Fo-Doh Laba.

Kidunia, Togo wanashika nafasi ya 124 katika viwango vya ubora wa Fifa ambavyo vilitangazwa kwa mara ya mwisho mwezi Oktoba, lakini Comoro iko katika nafasi ya 142.

Misri 1-1 Kenya

Matokeo ya kushangaza katika kundi hilo hayakuishia kwa mchezo wa Togo dhidi ya Comoro.

Kenya ikiwa ugenini nchini Misri huku wengi wakimpa nafasi kubwa mwenyeji kuibuka na ushindi, ililazimisha sare ya bao 1-1 katika mechi hiyo iliyochezwa ndani ya dimba la Borg El Arab jijini Alexandria, Alhamisi.

Misri inashika nafasi ya 49 kidunia katika viwango vya ubora vya Fifa wakati Kenya iko katika nafasi ya 108.

Wenyeji walikuwa wa kwanza kufunga bao kupitia kwa Mahmoud Kahlaba katika dakika ya 42 na Kenya walisawazisha kupitia kwa Michael Olunga katika dakika ya 67.

Angola 1-3 Gambia

Angola iko katika nafasi ya 120 kwenye viwango vya ubora vya Fifa, lakini ilijikuta katika mshtuko baada ya kuchapwa nyumbani kwa mabao 3-1 na Gambia ambayo iko katika nafasi ya 166.

Mechi hiyo ilichezwa Jumatano iliyopita katika Uwanja wa Novemba 11 jijini Luanda.

Mabao mawili ya Assan Ceesay na moja la Sulayman Marreh yalitosha kuipa ushindi huo Gambia wakati bao moja la Angola likifungwa na Wilson Eduardo.

Ikumbukwe kwamba hii siyo mara ya kwanza kwa Lesotho kufanya kitu kama hicho kwani mwaka 2017 iliwahi kulazimisha sare kama hiyo dhidi ya Taifa Stars katika mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu Afcon uliochezwa katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Sierra Leone 1-1 Lesotho

Lesotho iliingia katika mchezo wa ugenini dhidi ya Sierra Leone uliochezwa Jumatano iliyopita jijini Freetown huku wenyeji wakiwa na kikosi kilichojaza idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Hata hivyo, taifa hilo dogo kutoka kusini mwa Afrika liliwakomalia wenyeji na kutoka nao sare ya bao 1-1 wakifunga bao kupitia kwa Jane Thabantso wakati lile la Sierra Leone likifungwa na Kwame Quee

Kwenye viwango vya ubora wa soka, Sierra Leone iko nafasi ya 117 wakati Lesotho inashika nafasi ya 138.