Matumla ampa ushauri bondia Mwakinyo

Muktasari:

  • Mwakinyo amepanda hadi nafasi ya 18 kwa mujibu wa rekodi zilizotolewa na mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) kwenye uzani wa super welter wiki hii.

Dar es Salaam. Licha ya kupanda kwenye viwango vya ngumi vya dunia, bondia Hassan Mwakinyo amepewa angalizo ili kuendelea kubaki katika ubora wake.

Mwakinyo amepanda hadi nafasi ya 18 kwa mujibu wa rekodi zilizotolewa na mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) kwenye uzani wa super welter wiki hii.

Awali, Mwakinyo alizichapa na Sam Eggington wa Uingereza aliyekuwa bondia wa nane wa dunia na kumchapa kwa TKO, pambano lililompandisha hadi nafasi ya 19 mwaka jana.

Baada ya pambano la Uingereza, Mwakinyo alipigana na Joseph Sinkala ambaye ni wa bondia wa 407, Said Yazidu wa 538 na Muargentina, Sergio Eduardo Gonzalez ambaye ni bondia wa 215 na kushuka hadi nafasi ya 22 kabla ya wiki hii kupanda hadi nafasi ya 18.

Hata hivyo, kupanda viwango kwa Mwakinyo hakutokani na rekodi ya mapambano aliyopigana baada ya lile la Uingereza, isipokuwa mabondia waliokuwa juu yake walipoteza mapambano yao na kushushwa pointi.

Kauli za wadau

Licha ya Mwakinyo kusisitiza ana mkakati wa kucheza pambano kubwa la kimataifa mwaka huu, wadau wa ngumi wamemshauri kucheza na mabondia wa kiwango chake ili kuongeza thamani yake huku wakitaja mambo matano ambayo yanaweza kumshusha Mwakinyo kama asipojipanga.

Bondia bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla ambaye ana historia ya kuingia kwenye ‘Top 20’ ya dunia alisema ili bondia aendeleze kiwango anapaswa kucheza mara kwa mara.

Matumla alisema yeye hadi kufika katika rekodi ya kuwa bondia wa 20 bora alishinda mapambano ya ubingwa wa dunia ya WBU, UBO na baadhi ya mikanda ya Afrika .

Promota wa ngumi nchini, Shomari Kimbau alisema tangu Mwakinyo alivyompiga Eggington hakuwahi kupigana na bondia ambaye yuko kwenye ‘Top 50’ au pambano la ubingwa mkubwa.

Kimbau alidai Mwakinyo hajatumia thamani yake kupata faida inayoendana na kiwango chake.

Kuporomoka

“Amepanda lakini si kama anacheza mapambano ya kumpandisha, isipokuwa wale waliokuwa juu yake katika viwango wanapoteza hivyo pointi zao zinapungua yeye anapata nafasi ya kupanda kutokana na mtaji wa pointi zake,” alisema kocha nguli wa ngumi, Habibu Kinyogoli.

Mwakinyo afunguka

Mwakinyo ambaye yuko chini ya udhamini wa kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa Tanzania, alisisitiza yuko katika maandalizi ya kucheza pambano alilodai litakuwa kubwa ambalo anaamini litampandisha katika rekodi na amewataka wadau wa mchezo huo kumuunga mkono.