Maxime: Kutua Yanga ni suala la muda tu

Mwanza. Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema ishu ya kutua Yanga ni suala la muda iwapo vigogo wa Jangwani watakamilisha baadhi ya vipengele kwenye mkataba waliompa.

Maxime ambaye amekuwa msumbufu hasa timu yake inapokutana na vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga, alitajwa tangu mwanzoni mwa msimu huu kutua Jangwani lakini dili lake lilishindwa kukamilika kwa kutotimiza baadhi ya masharti.

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ameiwezesha Kagera Sugar kushika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 41 baada ya mechi 29.

Akizungumza na Mwananchi jana, Maxime alisema ana mkataba wa Yanga na anachosubiri ni kukamilika kwa baadhi ya vipengele na masharti aliyowapa ili kuungana nao kikosini.

Alisema kwa sasa bado ni mali halali ya Kagera Sugar, lakini iwapo Yanga watafuata taratibu zote hana tatizo kutua kwenye timu yake hiyo ya zamani.

“Lolote linawezekana inamaana hata kesho naweza kuungana nao kama viongozi wa Yanga watakamilisha baadhi ya vipengele kwenye mkataba walionipa, ila mimi kwa sasa ni mali ya Kagera Sugar” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, alisema kazi yake ni kufundisha soka, hivyo hawezi kuchagua timu ya kufanya nayo kazi kama maslahi na mazingira yatakuwa rafiki kwahiyo sina ubaguzi wa timu,” alisema kocha huyo.