Mbelgiji Yanga atoa sababu za kipigo

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Luc Eymael amekaribishwa kwa kipigo baada ya timu yake kufungwa mabao 3-0 na Kagera Sugar.

Eymael raia wa Ubelgiji, jana ilikuwa mechi yake ya kwanza kukaa katika benchi tangu alipokabidhiwa mikoba ya Mwinyi Zahera.

Akizungumzia kipigo hicho, Eymael alisema yametokana na makosa ya mabeki aliodai walifanya makosa matatu yaliyowagharimu.

Kocha huyo alisema mabeki walishindwa kujipanga vyema hatua iliyotoa nafasi kwa Kagera kuliandama lango lao mara kwa mara.

“Ni makosa ya kiufundi yaliyofanywa na mabeki, walitoa mwanya kwa Kagera, si kwamba walicheza vibaya, walifanya makosa matatu ambayo yametugharimu,”alisema Eymael.

Mabeki wa kati Kelvin Yondani na Lamine Moro walicheza kwa kutoelewana hatua iliyotoa nafasi kwa Yusuf Mhilu na Kelvin Sabato kuwapenya mara kwa mara.

Yondani na Lamine walifanya makosa ya mara kwa mara ambayo yalimuweka katika mazingira magumu kipa Farouk Shikalo.

Mhilu ambaye amewahi kucheza Yanga kabla ya kutemwa, aliwatoka mabeki hao ambao walishindwa kumdhibiti.

Pia alisema Yanga ilikuwa na nafasi nzuri ya kufunga idadi kubwa ya mabao, lakini washambuliaji wake walikosa umakini walipoingia ndani ya eneo la hatari la Kagera.

Alisema tangu makosa ya safu ya ulinzi na ushambuliaji alianza kuyabaini mapema katika mazoezi, lakini ataendelea kuyafanyia kazi.

“Si kwamba Kagera ni timu bora sana kuliko Yanga, walipata nafasi wakazitumia,”alisema kocha huyo ambaye wakati wa mapumziko alimsogelea mwamuzi wa mchezo huo timu zilipokuwa zikienda vyumbani.

Awali, Eymael alisema haifahamu Kagera lakini amejipanga kupata ushindi kwa kuwa amepata taarifa zao kupitia kwa wasaidizi wake.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo alipoanza kuinoa timu hiyo kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Dar es Salaam.

Wakati Eymael akitoa sababu za kipigo, kocha wa Kagera Mecky Maxime alisema wametumia udhaifu wa Yanga katika eneo la ulinzi kufunga mabao hayo.

Maxime alisema baada ya kupoteza mechi tatu zilizopita, walijipanga kushinda mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Safu ya kiungo ya Yanga ilipwaya na kufanya idadi kubwa ya wachezaji wa Kagera kumiliki mpira kwa muda mrefu sanjari na kutengeneza mashambulizi mengi. Mabao ya Kagera katika mchezo huo yalifungwa na Yusuh Mhilu, Ally Ramadhani na Peter Mwalyanzi.