Mbelgiji afichua siri Yanga

Muktasari:

Kocha wa Yanga Luc Eymael amesema ana matumaini ya kupata mafanikio kimataifa

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga Luc Eymael amesema amevutiwa na viwango vya wachezaji wake aliodai wana uwezo wa kuipa mafanikio klabu hiyo katika soka la kimataifa.

Akizungumza kwenye mazoezi Dar es Salaam jana, Eymael alisema amevutiwa na kiwango cha mchezaji mmoja mmoja baada ya kuwafundisha kwa mara ya kwanza.

“Nimevutiwa na uwajibikaji wa kila mchezaji, nimeona wachezaji wote ni wazuri ninaweza kufanya nao kazi, nataka kuifanya Yanga kuwa timu bora kupitia hawa niliowakuta,”alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji. Kocha huyo aliyejaza nafasi ya Mwinyi Zahera, alisema alianza kuvutiwa na kazi nzuri ya wachezaji hao katika mchezo dhidi ya Simba waliotoka sare ya mabao 2-2 Januari 4.

“Si jambo rahisi timu kurudisha mabao mawili katika mchezo wa timu pinzani, nilivutiwa na morali yao. Kwa wachezaji niliowakuta sioni sababu ya kufumua kikosi, labda nitarekebisha kasoro ndogo tu za kiufundi,”aliongeza Eymael.

Kocha huyo alisema anataka kuisuka Yanga mpya ambayo itakuwa alama kwa klabu za Afrika kwa ubora kwa kuwa ana timu imara.

Hata hivyo, Eymael alisema kila mchezaji anatakiwa kuwajibika ipasavyo ili kupata namba katika kikosi cha kwanza.

Katika mazoezi hayo Eymael alikuwa na aliyekuwa kaimu kocha mkuu Charles Mkwasa kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Dar es Salaam ambapo alionekana akihimiza wachezaji kutumia pasi fupi kuanzia kwa mabeki hadi washambuliaji.

Kocha huyo alipenda kutumia mfumo wa 3-5-2 ingawa mara chache alitumia 4-4-2 katika kufundisha.