Mbelgiji kumbe anawataka hawa Simba

Sunday June 9 2019

 

By MWANAHIBA RICHARD

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems yupo kwao Ubelgiji kwa mapumziko, akiwa amekabidhi ripoti yake ya msimu mzima kwa mabosi wake ikiwemo mapendekezo ya usajili wa msimu ujao, akiainisha nyota sita anaowataka kwa kikosi cha msimu ujao.

Katika ripoti hiyo imeelezwa Mbelgiji huyo upande wa usajili amewaeleza mabosi wake anahitaji ufanyike usajili wa wachezaji zaidi ya wanane ambao wataingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na wasiwe wachezaji wa kujaribiwa.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kati ya wachezaji anaowataka kocha wao ni wachezaji wanne wa kigeni, huku wawili ambao ni wazawa.

Kimbembe kipo kwa nyota wa kigeni wanaodaiwa bado hawajapata nyota atakayefaa kuichezea Simba inayohitaji mafanikio makubwa baada ya kushindwa kumpata nyota wa Zesco ya Zambia, Lazarous Kambole ambaye dau lake liliwashinda Simba.

Faili la usajili wa Simba lipo njia panda ili kupitisha panga kwani nyota wanaotajwa kwenye mpango wa kutemwa, wageni wakiwemo Paschal Wawa, James Kotei, Emmanuel Okwi, Nicholas Gyan na Haruna Niyonzima japo baadhi wanaonekana bado wanahitajika.

Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika toka Simba Aussems ametaka kipa mpya wa kusaidiana na Aishi Manula kwani Deo Munishi ‘Dida’ anaondoka, beki namba tatu, beki wa kati wawili, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji, winga ya kulia na mastraika.

Advertisement

Chanzo hicho kimeliambia Mwanaspoti kwa upande wa wachezaji wa ndani, Aussems amempendekeza Ramadhan Kapera wa Kagera Sugar pamoja na beki Kennedy Juma wa Singida United.

“Kila siku mambo ya usajili yanazungumzwa kilichobaki ni utekelezaji tu, hatuwezi kukurupuka kwasababu tu wenzetu wanasajili ni lazima tutulize akili tunapoangalia mchezaji wa kuitumikia Simba kwa mafanikio makubwa.

“Unapowapunguza wachezaji ni lazima usajili ambao ni bora zaidi ya wale walioondoka, hivyo sio jambo la kufanya pupa hasa kwa wachezaji wa kigeni, hawa wetu wazawa ni rahisi maana kocha amewahitaji moja kwa moja aliporidhishwa na viwango vyao,” alisema mjumbe huyo.

Kuhusu wachezaji watakaotemwa alisema: “Ukipata wachezaji ndio unaweza kuwatema wachezaji, hivyo mchakato unaendelea kwani hata muda wa kusajili bado upo,”

Alisema usajili wa mchezaji wa Ndanda, Vitalis Mayanga waliyemsajili dirisha dogo na Salum Kihimbwa wa Mtibwa Sugar umepigwa chini kwani imedaiwa kocha amewaambia mabosi wake kuwa viwango vyao havina tofauti na wazawa waliopo kwa sasa Simba.

Mjumbe huyo alifafanua kwa nafasi ya kiungo mkabaji inayochezwa na Jonas Mkude pamoja na James Kotei pia anaongezwa nguvu na hapo yatafanyika maamuzi kulingana na ubora wa nyota atakayepatika kumsajili.

MBONDE, BUKABA KWA MKOPO

Chanzo hicho kimeweka wazi kuwa, baadhi ya wachezaji watapelekwa kwa mkopo timu nyingine akiwemo Salum Mbonde ambaye hakuwa na msimu mzuri kutokana na majeraha.

Mbali na Mbonde imeelezwa hadi sasa mchezaji mwingine anayeweza kupelekwa kwa mkopo ni Paul Bukaba.

MKWABI AFUNGUKA

Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alisema kila kinachofanyika ndani ya klabu yao kitatolewa taarifa rasmi mara kitakapokamilika na sio kuzungumzia tetesi.

“Sio rahisi kuweka wazi mipango ya klabu ikiwemo mambo ya usajili, haya mambo yatawekwa wazi huko mbele yatakapokuwa tayari, kwasasa tuache watu wafanyekazi yao.”

Advertisement