Mchezaji wa Cardiff ahofia kufariki katika ajali ya ndege

Muktasari:

  • Mchezaji huyo mwenye uraia wa Argentina alisaini mkataba wa kuichezea Cardiff Jumamosi na alikuwa akisubiri kuanza mazoezi na wachezaji wenzake wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England


Mshambuliaji aliyeweka rekodi ya kusajiliwa kwa donge nono katika klabu ya Ligi Kuu ya Cardiff City, Emiliano Sala ambaye ni raia wa Argentina, alikuwa kwenye ndege ndogo ambayo ilitoweka katika duru za Uingereza usiku wa kuamkia jana, polisi wameiambia AFP.
Sala, aliyesaini kuichezea Cardiff Jumamosi akitokea klabu ya Ufaransa ya Nantes kwa ada ya dola 19.3 milioni za Kimarekani, alikuwa akienda Cardiff kwa ndege ndogo, ambayo ilipotea kutoka katika rada za ikiwa kilomita 20 kkaskazini mwa Guernsey, mtu ambaye hakutaka jina lake lifahamike, alisema.
Taarifa ya polisi wa Guernsey, kisiwa cha Uingereza kilicho karibu na pwani ya Ufaransa, alisema boti za uokoaji na helikopta ziliitafuta kwa saa kadhaa ndege hiyo, ambayo ilikuwa na abiria wawili na kepteni.
"Utafutaji huo ulisitishwa saa 08:00 usiku wakati vifaa vyote viliposimamishwa kutokana na kuongeeka kwa upepo, kuchafuka kwa bahari na uwezo hafifu wa kuona," ilisema taarifa hiyo.
"Hadi wakati huo, hakukuwa na dalili za kuiona ndege," iliongeza.
Helikopta mbili, ndege mbili na boti za uokoaji ziliingia katika jitihada mpya za utafutaji leo asubuhi kuitafuta ndege hiyo yenye injini moja ya pangaboi ambayo inadhaniwa ilipata ajali.
Sala, 28, ambaye amekuwa Nantes tangu mwaka 2016 na ambaye alifunga mabao 13 katika mashindano tofauti msimu huu, alisaini mkataba wa miaka mitatuy na nusu katika klabu ya Cardiff ambayo inakabiliwa na tishio la kushuka daraja, lakini usajili wake unasubiri kibali cha kimataifa.
Hakuna klabu iliyozungumzia suala hilo, lakini Nantes imeahirisha mechi yake ya Kombe la Ufaransa dhidi ya timu ya daraja la tatu ya Entente SSG iliyopangwa kufanyika kesho kuonyesha heshima yake.
Aliposaini mkataba wa kuichezea Cardiff Jumamosi, Sala, ambaye pia ana uraia wa Italia, alisema katika taarifa yake: "Ninafurahia kuwa hapa. Inanifanya nifurahie na natamani kuanza mazoezi, nikutane na wachezaji wenzangu wapya na kuanza kazi."