Mchongo kamili wa Stars AFCON ni huu

Dar es Salaam. Mbinu ya kujilinda katika sehemu kubwa ya mchezo na kushambulia kwa kushtukiza iliyotumiwa na Taifa Stars dhidi ya Mafarao wa Misri katika mechi ya kirafiki juzi, imeakisi kile alichodhamiria kufanya kocha Emmanuel Amunike katika Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazoanza Juni 21 nchini Misri.

Stars ilicheza kwa ‘jihad’ ikiwabana wenyeji katika mechi hiyo ya kirafiki waliyolala 1-0 na wageni wangeweza kupata japo sare katika angalau nafasi tatu walizozipata katika kipindi cha pili.

Tanzania iliyowaanzisha washambuliaji watatu nahodha Mbwana Samatta, John Bocco na Saimon Msuva, haikuingia tamaa ya kufunguka ovyo kwa kuwaheshimu wapinzani na muda mwingi washambuliaji hao walirudi nyuma kusaidia ulinzi.

Mfumo wa 5-4-1 unaonekana unaweza kuwa chaguo sahihi kwa benchi la ufundi la Stars kuutumia kwenye mechi ya ufunguzi wa AFCON kwa Tanzania dhidi ya timu inayoshika namba moja ya ubora wa viwango vya soka barani Afrika, Senegal inayoongozwa na mdunguaji hatari, Sadio Mane.

Ifahamike kwamba Senegal pindi wanapokabiliana na timu ya wastani au ya daraja la chini, imekuwa ikitumia mfumo wa 4-3-3 ambao unakuwa na washambuliaji watatu na viungo washambuliaji wawili au ule wa 4-4-2 ambao unakuwa na washambuliaji wawili, mawinga wawili na kiungo mmoja mshambuliaji.

Lakini katika mchezo wa pili dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’, Taifa Stars haina haja ya kukaa nyuma na kujilinda na badala yake inaweza kufunguka kwa kucheza 4-3-3 ikiwa na washambuliaji watatu ama ikatumia mfumo wake wa 4-4-2 kwani majirani zao wamekuwa wakitumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao unakuwa na viungo wawili wakabaji wanaosaidiwa na mawinga wawili na kiungo mmoja mshambuliaji juu yao huku mshambuliaji wa kati akisimama mmoja tu ambaye huwa ni Michael Olunga ingawa kuna wakati hucheza 4-4-2 yenye mawinga wawili na washambuliaji wawili.

Mchezo dhidi ya Algeria, Stars inaweza kucheza mfumo wa 4-5-1 ama 4-4-2 lakini wachezaji watakaopangwa kucheza kama mawinga au viungo wa pembeni watapaswa kufanya kazi kubwa ya kuwasaidia mabeki wao namba mbili na tatu kwani Algeria kama ilivyo asili ya timu za kutoka Kaskazini mwa Afrika imekuwa ikishambulia na kuzalisha idadi kubwa ya mabao kutokea pembeni.

Na silaha ambazo Algeria imekuwa ikizitumia zaidi ambazo zinacheza pembeni ni mastaa wake wawili, Yacine Brahimi na Riyad Mahrez ambao ndiyo walichangia kwa kiasi kikubwa kuiteketeza Stars katika kipigo cha mabao 7-0 katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe Dunia za mwaka 2018 ambao ulichezwa Novemba 17, 2015.

Mchambuzi wa soka, Alex Kashasha alisema kiwango kilichoonyeshwa na Stars kwenye mchezo wa juzi kinatoa ishara nzuri kuelekea mechi zijazo za AFCON.

“Kwa ujumla mechi ilikuwa ngumu kwa sababu tatu nazo ni Misri ni timu bora Afrika na ipo juu kwa muda mrefu, pili tumecheza na mabingwa mara saba wa AFCON lakini tatu tumekutana na wapinzani ambao wana kundi kubwa la wachezaji wa daraja la juu hivyo jambo la msingi mwalimu ambalo nimeliona alilenga ni kuona ni jinsi gani timu inaweza kujilinda na ndiyo maana umeona mawinga ambao ni Bocco na Farid Musa muda mwingi walikuwa wanashuka kusaidia mabeki wao wa pembeni, jambo lililozaa matunda na kweli timu ikafanikiwa kutimiza mpango huo kwani hata kwenye viungo, wote walianza wale ambao wanacheza mbele ya mabeki.

“Naamini kwenye mechi dhidi ya Senegal na Algeria staili hii itatusaidia lakini kwenye mchezo dhidi ya Kenya sidhani kama tutaingia kwa staili hiyo na naamini tutashambulia,” alisema Kashasha.

Kipa Aishi Manula alisema kuwa mchezo wa juzi dhidi ya Misri umewapa darasa tosha katika maandalizi yao kabla ya fainali hizo.

“Ni mechi ambayo tumecheza dhidi ya timu nzuri na naamini imesaidia kutujenga katika kibarua ambacho kipo mbele yetu,” alisema Manula.

Stars itacheza mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe, kesho Jumapili kabla ya kuanza kwa fainali za AFCON.