Mhina akumbuka tishio la mashabiki kumchomea nyumba

Mwanza. Mlinda mlango wa zamani wa Pamba, Yanga na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Juma Mhina amesema licha ya kwamba amestaafu soka miaka mingi, hawezi kusahau tukio la mwaka 1989 alipotishiwa kuchomewa nyumba na mashabiki wa Pamba baada ya kufungwa bao na Malindi FC kwenye Fainali ya Kombe la Muungano.

Katika mchezo huo, Malindi ilishinda kwa bao 1-0.

Akizungumza katika mahojiano maalumu juzi Mhina alisema tukio hilo lilimuathiri kisaikolojia na kumfanya akae nje ya uwanja kwa takribani miaka minane.

Kwa sababu hiyo, aliwataka mashabiki wa soka nchini kutoingia uwanjani wakiwa na matokeo kwa sababu huwaathiri kisaikolojia pale inapotokea yakawa tofauti.

“Siwezi kusahau tukio la mwaka 1989 nilipofungwa bao la penalti dhidi ya Malindi FC kwenye fainali ya Kombe la Muungano,” alisema.

Alisema Pamba iliingia fainali baada ya kuzifunga Simba na Small Simba ya Zanzibar na ndipo ilipokutana na Malindi kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Alisema siku hiyo mashabiki walifurika na waliamini kwamba Pamba lazima itabeba ubingwa lakini mambo yalipobadilika walimtuhumu kuwa ameuza mechi.

Anasema bila ya kumpa fursa ya kujitetea, mashabiki hao walipandwa na hasira na kutishia kwenda kumchomea nyumba yake, suala ambalo lilipoa baada ya kamanda wa polisi na mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuingilia kati.

Alisema kitendo hicho kilimvuruga na kuamua kupumzika kwa msimu mmoja kabla ya kutimkia Shabana FC ya Kenya.

“Nilikosa furaha na amani na nikaona mpira hauna faida nikakaa nje. Mwaka 1990 Pamba inabeba ubingwa mimi sikuwapo kutokana na akili yangu kuvurugwa,” alisema kipa huyo aliyekuwa katika kikosi cha Tanzania kilichofuzu kuingia Fainali za Mataifa ya Afrika ‘Afcon’ mwaka 1980 kwa mara ya kwanza.

Katika hatua nyingine, mkongwe huyo amempongeza Rais John Magufuli kutoa zawadi kwa wachezaji waliowezesha Tanzania kufuzu fainali za Afcon, itakuwa na manufaa kwa nchi.

Nyota huyo ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Tanzania kwa mara ya kwanza kufuzu Afcon mwaka 1980 kuanzia hatua ya makundi.

Mhina alisema Tanzania ilichukuwa muda mrefu kufuzu kutokana na walioiwezesha kutopewa hata shukrani.

Alisema hatua ya Rais Magufuli kuwapa zawadi ya viwanja na pesa tasilimu wachezaji walioipeleka Tanzania kwenye fainali hizo kwa mara ya pili, itasaidia sana kwani itawapa morari ya kupambana kuipa mafanikio nchi.

“Mimi nilishiriki kuanzia hatua za makundi licha ya kwamba sikwenda Nigeria kwenye Fainali, lakini wachezaji hatukupewa

chochote kwahiyo alichofanya Rais Magufuli kitakuwa na manufaa kwa Tanzania,” alisema Mhina.