Minziro abeba matumaini ya Arusha

Sunday August 12 2018Kocha Fred Minziro.

Kocha Fred Minziro. 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Arusha. Wadau na mashabiki wa soka wa jiji la Arusha, pamoja na viongozi wa timu ya Arusha United wameweka matarajio makubwa ya kupanda daraja msimu huu.

Wadau hao ni kama wamembebesha mzigo Kocha wao Mkuu Fred Minziro, wakiamini ataiwezesha timu hiyo kupanda daraja kutokana na rekodi yake nzuri ya kuzipandisha daraja timu anazozinoa.

Minziro aliyezinoa timu kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara zikiwemo Yanga na JKT Ruvu aliyoipa mafanikio makubwa, ndiye aliyezipandisha daraja Singida United na KMC ya Kinondoni kutoka Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) kwenda Ligi Kuu.

Hilo ndilo linalowafanya wadau hao kuamini kuwa Arusha United itapanda daraja msimu huu kwa kuwa ipo katika mikono salama ya Minziro.

Kikosi hicho chenye wachezaji 27 kinatarajiwa kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi hapo kesho chini ya Kocha msaidizi Fikiri Elias, kutokana na Kocha Mkuu Minziro, kutokuwepo.

Alisema awali timu hiyo ilitakiwa kuanza kambi Agosti 2, lakini kutokana na ligi hiyo kusogezwa mbele hawakuona sababu ya kuanza mazoezi mapema, hivyo wakawapa wachezaji likizo ya wiki mbili zaidi.

Advertisement

“Katika usajili wetu tuna jumla ya wachezaji 27, kati yao wanne wamecheza Ligi Kuu tunaamini watatusaidia sana, Kocha Mkuu Fred Minziro, atakaporejea kutoka Bukoba alikokwenda kwa matatizo ya kifamilia ataweka wazi programu tutakayoanza nayo,” alisema Elias.

Timu hiyo itaanza mazoezi katika uwanja inaoutumia kama uwanja wake wa nyumbani wa General Tyre uliopo Njiro nje kidogo ya jiji la Arusha, ukiwa karibu na makazi ya timu hiyo yaliyopo kwenye viwanja vya Nane nane.

Advertisement