Minziro ataja sababu kuachwa na timu nne

Dar na Mwanza. Wakati akisikilizia hatima yake ndani ya Alliance FC, Kocha Fred Felix Minziro ameanika sababu za kuachwa na timu nne katika kipindi kifupi.

Uongozi wa Alliance FC umefanya mabadiliko ya benchi la ufundi na kumrejesha Kessy Mzirai kuwa kocha mkuu, huku Minziro akisubiri kupangiwa majukumu mengine.

Alitua Alliance msimu huu, alitokea Singida United ya Ligi Kuu na Pamba ya Mwanza inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza. Kabla ya kufundisha timu hizo, kocha huyo alitokea Arusha United ya Ligi Daraja la Kwanza aliyoifundisha msimu uliopita.

Aliajiriwa na Alliance FC miezi kadhaa iliyopita akichukua mikoba ya Mziray ambaye alijiengua kikosini kwa madai ya ugonjwa muda mfupi baada ya Alliance kumleta Minziro, sasa kocha huyo atasaidiwa na Gilbert Dady.

Ofisa Habari wa Alliance, Jackson Mwafulango alisema hivi karibuni kuwa Minziro atapangiwa majukumu mengine na aliyekuwa msaidizi wake, Mathias Wandiba amepelekwa kunoa timu ya vijana (U-20).

Akizungumzia kuwekwa kando kwenye nafasi ya ukocha mkuu wa timu hizo ikiwamo Alliance ambayo ameiongoza katika mechi 15, kati ya hizo mbili za FA na kushinda nne, sare nne za kufungwa saba, Minziro alisema haoni tatizo kwani makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe.

“Arusha United kulikuwa na mkakati wa kuipandisha, ikashindikana, timu ikamaliza ya tatu, Singida United ndiyo niliipandisha daraja kucheza Ligi Kuu, tukashindwana nikaondoka, baadaye wakanirudisha,” alisema.

Alisema katika timu ya Pamba pia kuna vitu walishindwa kuelewana ndiyo sababu aliamua kutimka na kwenda Alliance FC.

“Alliance hawajaniambia lolote kuhusu kuleta kocha mkuu na mimi kunipangia majukumu mengine, acha niwasikilize kwanza kama ni kweli ndipo nitajua nini cha kufanya,” alisema.

Kocha huyo ambaye ana historia ya kuzipandisha timu kucheza Ligi Kuu, alisema hana hofu ya kutupiwa virago na Alliance FC kwani soka ndivyo lilivyo.

Alliance FC inashika nafasi ya tatu kutoka mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 29 katika mechi 29 ilizocheza na inakabiliwa na hatari ya kushuka daraja kama ilivyo kwa Singida United inayokamata mkia, Mbao, Mbeya City, Ndanda na KMC. Timu nne zitashuka moja kwa moja wakati mbili zikicheza mtoano (playoff).

Wakizungumzia Minziro kwa nyakati tofauti, Kocha Kenny Mwaisabula na mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Iddi Kipingu walisema ni kocha mzuri, lakini anapaswa kujitathimini.

“Nimewahi kusoma naye kozi mbili tofauti za ukocha, yuko vizuri mno, ni mhamasishaji pia. Kinachomtokea huenda kinasababishwa na tabia zake kwa uongozi,” alisema Mwaisabula.

Alisema kinachomtokea kila mara kocha huyo hata yeye kinamuachia maswali, kwani amekuwa na historia ya kufikisha timu katika hatua nzuri ikiwamo kuzipandisha daraja, lakini baada ya muda anaondolewa.

“Haiwezekani kila timu inamuacha, tena baadhi ya timu hakai muda mrefu, nachelea kusema hii inachangiwa na namna anavyoishi na timu hizo, lakini si kiwango chake kwani namfahamu katika sekta ya ukocha yuko vizuri,” alisema.

Kipingu alisema kwa hali ilivyo, inabidi Minziro ajitathmini mwenyewe kuona tatizo liko wapi hadi timu nyingi zinaishia kuachana naye katika mazingira kama hayo.

Kurudi Pamba

Wakati akisubiri kujua hatima yake Alliance FC, Minziro huenda akarudi kwenye timu yake ya zamani ya Pamba.

Kaimu Katibu Mkuu wa Pamba, Johnson James alisema suala la kurejea kwa Minziro si baya kwani ni kama anarudi nyumbani na linasimamiwa na kamati maalumu.

“Hilo suala la Minziro lipo chini ya kamati maalumu ambayo itatupa taarifa ya nini kifanyike, lakini pia huyu kocha ni kama anarudi nyumbani kwa sababu alishainoa Pamba na kazi yake tunaijua,” alisema James.

Alipoulizwa kuhusu kurejea katika kikosi hicho cha jijini Mwanza, Minziro alisema kuwa licha ya kwamba hajapewa taarifa za kurudi Pamba, lakini yupo kwa ajili ya kazi ya kufundisha mpira, hivyo yuko tayari kwa lolote.