Mkijichanganya tu, tunawamaliza tena

Thursday April 25 2019

 

By SADDAM SADDICK, MWANZA NA THOBIAS SEBASTIAN, DAR

USHINDI wa mabao 2-0 iliyopata Simba juzi Jumanne dhidi ya Alliance umempa mzuka Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems akisisitiza kuwa KMC wanaovaana nao leo Alhamisi wakijichanganya tu wanawaumiza tena, huku wapinzani wao wakicheka kwa dharau wakisema hata wao wanataka ushindi.

Kocha Aussems amesema kuwa wanahitaji alama tatu katika mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ili kuzidi kuweka hai matumaini ya kutetea taji, lakini mabosi wa KMC wakisema Simba wasitarajie mteremko tena kwani hata wao wanazitaka alama tatu kujiweka pazuri.

Akizungumza na Mwanaspoti kuelekea mchezo wa leo, Kocha Aussems alisema licha ya ratiba kuwawia ugumu, mkakati wao ni kuendelea kupambana kuhakikisha kila mchezo wanavuna pointi tatu.

Kocha huyo alisema kutokana na hali ilivyo kwa sasa atakuwa akiwapanga wachezaji tofauti huku wengine wakipumzika ili kufikia malengo yao na kwamba anaamini Simba itatetea ubingwa wake.

“Ratiba ni kama unavyoiona ni ngumu kweli, hatuna namna tutaendelea kupambana kuhakikisha kila mchezo tunatafuta pointi tatu bila kuchoka,” alisema Aussems.

Kocha huyo aliongeza anaamini mchezo hautakuwa rahisi kutokana na ushindani uliopo baina yao na wapinzani wao hivyo wanapaswa kuwa makini kwa dakika zote 90.

MPANGO ULIVYO

Kocha Aussems alisema mpango wake wa kwanza ni kupangua kikosi katika kila mechi na kuwapa nafasi kila mchezaji kucheza kwani timu yake ina wachezaji 25, ambao wote wapo vizuri na kila ambaye atakuwa anapata nafasi ya kucheza ana imani hawatamuangusha kwani yupo nao mazoezini.

“Tangu mechi ya Coastal Union nimekuwa nikipangua kikosi na kuwapa nafasi wachezaji kama njia ya kuwapumzisha miili yao na kucheza kwa ushindani,” alisema.

Alisema kwa jinsi ratiba ilivyo hana muda wa kufanyisha mazoezi zaidi ya kurejesha miili katika hali yake (recovering) kwa wale wachezaji ambao watakuwa wametumika kwenye mchezo uliopita ili kuwa sawa na wale ambao watatumika katika mchezo unaofata kulingana na ratiba yao ilivyo.

“Natambua kila mechi itakuwa ngumu kwetu kulingana na ratiba yetu ilivyo ila imani yetu ni kuvuna pointi tatu katika kila mechi iliyokuwa mbele yetu, pia niwashukuru mashabiki wetu kwa nguvu na mshikamano wao wanaoonyesha kokote tunapocheza, kwani hata mechi ya KMC hali itakuwa hivyo.”

Nahodha John Bocco alisema kimsingi wana ratiba ngumu inayowakabili kipindi hiki inayowahitaji kucheza mechi kila baada ya siku mbili mpaka tatu, hivyo wachezaji wanatakiwa kuwa kiushindani zaidi ya hapo awali.

Bocco alisema benchi la ufundi limeliona hilo na litakuwa linawapa mbinu na hata mabadiliko ambayo yanafanyika katika kila mechi anaungana nayo ili kutoa nafasi kwa wachezaji wengine kupumzika na kwamba wale ambao wanapata nafasi ya kucheza hawatafanya mzaha hata kidogo.

KMC HAWATANII

Pamoja na Simba kujinadi kuzitaka alama zote tatu kutoka kwa KMC, Meneja wa timu hiyo, Faraji Muya alisema kikosi kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo na matarajio yao ni ushindi.

Alisema wachezaji walio kwenye mpango wa kocha wako vizuri kisaikolojia na morali hivyo pointi tatu ni muhimu katika harakati zao za kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo na kwamba watakuwa makini kuwadhibiti wapinzani hao.

KMC ipo nafsi ya saba ikiwa na alama 42 baada ya mechi 32, ina kazi ya kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Desemba 19 mwaka jana, lakini pia ikitaka ushindi ili kurejea kwenye Nne Bora baada ya kuporomoshwa na matokeo ya timu nyingi zinazoshiriki ligi hiyo.

Katika mchezo wa leo Alhamnisi KMC huenda ikawakosa baadhi ya nyota wake kutokana na majeruhi na kuwa na kadi wakiwamo washambuliaji wao matata, japo Kocha Mkuu wao, Etienne Ndayiragije amesisitiza kuwa vijana wake wapo tayari kwa ajili ya kupambana na watetezi hao wa Ligi Kuu Bara.

Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama zao 63 baada ya mechi 25, ikiwa ni pointi tatu nyuma ya Azam waliopo juu yao na pointi 11 nyuma ya walizonazo watani zao, Yanga waliopo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kushuka uwanjani mechi 32 kila mmoja wakiwa na alama 74 .

Advertisement