Mkwasa aitingisha TFF, atishia kwenda Fifa

Kocha wa zamani wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Charles Mkwasa

Muktasari:

  • Kocha wa zamani wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ ametishia kuishitaki TFF Fifa

Dar es Salaam. Baada ya kusotea fedha zake Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tangu mwaka 2017, aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema atapeleka malalamiko Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kupata msaada.

Mkwasa aliifundisha Taifa Stars Juni 2015 hadi Januari 2017 kabla ya kuondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Mayanga.

Akizungumza na gazeti hili, Mkwasa alisema amefuatilia fedha hizo bila mafanikio, hivyo anataka kuishirikisha Serikali au Fifa.

“Nilipoumwa nilikutana na rais wa TFF (Wallace Karia) nikamuomba wanipe fedha kidogo kati ya ninazodai ili zinisaidie katika matibabu, lakini ilishindikana,” alisema kocha huyo.

Ingawa hakutaka kuweka bayana kiasi cha fedha anazodai, Mkwasa alisema ni nyingi na nyingine ni malimbikizo ya malipo ya mishahara.

“Nimejaribu kwa namna zote kuona kama nitalipwa bila mafanikio hadi sasa nafikiria kwenda Fifa labda naweza kupata msaada,” alisema Mkwasa.

Alisema gharama ya matibabu yake India (alikofanyiwa upasuaji wa moyo mwaka jana) zililipwa na mkewe (Betty Mkwasa) na mdau wa Klabu ya Simba.

“Nilizungumza na rais (Karia) kabla sijaondoka kwenda India, sababu ile ni haki yangu na kazi nilifanya, lakini imeshindikana, nikaomba watumie njia ya kunilipa kidogo kidogo napo imekwama,” alisema Mkwasa.

Alisema mpaka TFF inasitisha mkataba wake Januari 2017 walikuwa wamelimbikiza malipo yake na alipoondoka waliahidi kumlipa, lakini hadi sasa zaidi ya miaka miwili amekuwa akisotea malipo hayo bila mafanikio.

“Walinifukuza kama walivyofanya kwa Amunike (Emmanuel) walisema wamefikia makubaliano na mimi kuvunja mkataba kama hivi walivyofanya kwa Amunike,” alisema Mkwasa.

Alisema TFF walimueleza watamlipa mshahara wa miezi mitatu kwa kuvunja mkataba na malimbizo ya nyuma aliyokuwa akidai atalipwa baada ya muda mfupi lakini imekuwa tofauti.

Rais wa TFF, Karia alipoulizwa jana madai ya Mkwasa, hakukanusha wala kukubali zaidi ya kusisitiza hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa Mkwasa ni kaka yake.

“Amekutuma uje uulize atalipwa lini? alihoji Karia na kueleza kwamba anaiheshimu familia ya Mkwasa na hawezi kuzungumza chochote kuhusu madai hayo.

“Sipendi kuongelea suala la Mkwasa na familia yake sababu ni watu wangu wa karibu, lakini nasikitika mno juu ya madai yake,” alisema Karia kwa kifupi jana.