Morrison ang’ara, Eymael roho kwatu

Singida: Kocha wa Yanga Luc Eymael ameshusha presha baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza jana, Eymael alisema ameridhika na kiwango cha wachezaji wake na amemtaja Benard Morrison ni mchezaji wa aina yake.

Morrison raia wa Ghana aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha dogo, alikuwa nyota wa mchezo baada ya kucheza kwa kiwango bora.

Eymael alisema Morrison amempa raha na alikuwa injini ya Yanga katika mchezo huo ambao timu hiyo jana ilikuwa ugenini kwenye Uwanja wa Liti.

Alisema Morrison alichangia kwa kiasi kikubwa matokeo hayo ingawa aliwapongeza wachezaji wote kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi. “Kama ningewahi usajili ningependa kuwa na wachezaji angalau wawili wa aina ya Morrison, amefanya kazi nzuri,”alisema Eymael.

Akizungumzia mchezo huo kiufundi, alisema Yanga ilikuwa na muunganiko mzuri katika idara zote na ana furaha kupata pointi tatu kwa kuwa Singida haikuwa timu ya kubeza.

“Uwanja haukuwa rafiki kwa timu zote, mpira ulikuwa ukidunda kutoka eneo moja kwenda jingine, lakini hiyo si sababu sana kwasababu kila mmoja ameona mpira,”alisema Eymael.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji alisema ana furaha kwa kuwa ametokea katika maumivu ya kufungwa mechi mbili mfululizo mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kulala bao 1-0 ilipocheza na Azam.

Kocha wa Singida Ramadhani Nsanzurwimo alisema anawajibika kubeba lawama ya matokeo mabaya ya timu hiyo kwa kufanya kosa la kuwaingiza wachezaji wawili ambao hawakuwa na msaada.

“Mimi ndio nawajibika timu haikucheza vizuri kuanzia mabeki, kati na washambuliaji. Nilifanya ingizo la wachezaji ambalo halikuwa na msaada,”alisema kocha huyo.

Yanga imeondoa nuksi kwenye uwanja huo ambao zamani uliitwa Namfua. Tangu Singida ipande Ligi Kuu mwaka 2017 imecheza na Yanga mara mbili ambapo zimetoka suluhu. Mechi ya kwanza Novemba 4 kabla ya kuvaana Februari 6, mwaka jana.

Mchezo wenyewe

Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya 12 lililofungwa na David Molinga kwa kifua baada ya Mapinduzi Balama kupiga kiki iliyomshinda kipa Owen Chaima.

Morrison alifanya kazi nzuri dakika ya 58 baada ya kuingia na mpira ndani ya 18 na kutoa pasi kwa Haruna Niyonzima aliyepiga kiki ya mbali iliyojaa wavuni.

Yanga ilipata bao la tatu dakika 76 lililofungwa na Yikpe Gnamien raia wa Ivory Coast kwa mpira wa kichwa baada ya kumzidi maarifa beki wa Singida aliyetaka kuokoa.

Dakika 83 Singida ilipata bao kupitia kwa Six Mwakasega ambaye alipata pasi ya mwisho iliyopigwa na kiungo nguli Athumani Idd ‘Chuji’.

Mbali na Chuji, Singida iliwatumia wachezaji beki wa kushoto Haji Mwinyi na kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ ambao waliwahi kucheza Yanga

Singida United: Owen Chaima, Aaron Lulambo, Haji Mwinyi, Daud Mbweni, Tumba Lui, Erick Mambo, Mashauri Kazungu, George Sangija, Elnyesya Sumbi, Haruna Moshi na Six Mwakasega.

Yanga: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jafari Mohammed, Lamine Moro, Said Makapu, Papy Tshishimbi, Deus Kaseke / Abdulaziz Makame, Haruna Niyonzima, David Molinga \ Yikpe Gnamein, Mapinduzi Balama na Bernad Morrison / Erick Kabamba.

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu uliochezwa jana, Azam iliichapa Mwadui ya Shinyanga bao 1-0 lililofungwa na Shabani Chilunda kwenye Uwanja wa Kambarage.

Azam imefikisha pointi 35 na ipo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu.