Msuva akoleza moto wa mabao Morocco

Dar es Salaam. Mshambuliaji Saimon Msuva amepania kuirejesha Difaa El Jadida ya Morocco katika michuano ya kimataifa msimu ujao.

Msuva alitoa kauli hiyo muda mfupi juzi usiku, baada ya kufunga bao muhimu katika mchezo wa Ligi Kuu Morocco ambao Difaa El Jadida ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Chabab Rif Hoceima.

Mchezaji huyo wa kimataifa, alisema pointi moja waliyopata dhidi wapinzani wao imewapaisha hadi nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu Morocco huku timu hiyo ikiwa imebakiwa na mechi mbili za mwisho.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, alisema mkakati ni kushinda mechi mbili zilizobaki ambazo zitawaweka katika mazingira mazuri ya kucheza michuano ya kimataifa.

Msuva alisema msimu huu ulikuwa na changamoto kwa upande wao kwa kuwa waliondokewa na baadhi ya nyota waliosajiliwa na klabu nyingine.

“Tunaelekea pazuri ukiangalia nafasi tuliyopo kuna tofauti ya pointi chache na timu ambazo zipo nafasi nne za juu, huku timu mbili za juu zinapata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa ya tatu ni itacheza shirikisho,” alisema Msuva.

Difaa El Jadida inashika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 38 ilizopata katika mechi 28. Msuva amefikisha mabao 13 msimu huu akizidiwa na Lajour Mouhssine wa Raja Casablanca, lakini amepachika wavuni 24 tangu alipojiunga na Difaa El Jadida.