Mwakinyo, Samatta watajwa bungeni

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge la 11 ambapo katika hotuba yake amewataka Watanzania kuelekeza dua zao kwa bondia Mwakinyo ili aweze kumgagadua mpinzani wake katika pambano lake Novemba 2019.

Dodoma. Mkutano wa 17 wa Bunge la 11 la Tanzania umeahirishwa hadi Januari 28, 2020 huku Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa akitaka duwa za Watanzania kwa bondia Hassan Mwakinyo ili amtwange bondi Mfilipino, Arnel Tinampay.

Leo Ijumaa Novemba 15, 2019 Bunge limekamilisha shughuli zake na kuahirishwa baada ya kukaa kwa wiki mbili.

Pamoja na kuwaombea wanamichezo wote ikiwemo timu ya taifa, Taifa Star inayoingia uwanja muda mfupi ujao leo kukabiliana na GUINEA YA Ikweta lakini Majaliwa amemuombea Mwakinyo amshinde mpinzani wake katika raundi ya kwanza.

"Watanzania wenzangu kwa pamoja tuungane kupeleka duwa zetu kwa bondia wetu ambaye mwisho wa mwezi huu atapanda ulingoni kuzichapa na Mfilipino, tumwombee amchape katika raundi ya kwanza tu," amesema Majaliwa huku akishangiliwa na wabunge

Kiongozi huyo pia amemtaja Nahodha wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samata kuwa ameendelea kuwatoa kimasomaso Watanzania kwa kuendeleza rekodi ya kufunga mabao katika mashindano makubwa.

Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi leo kuishangilia timu ya taifa na kuipa hamasa kubwa ili iweze kuibuka na ushindi.

Taifa Stars inacheza na Guinea ya Ikweta katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afron) 2021.

Taifa Stars ipo kundi J pamoja na Tunisia, Libya na Guniea ya Ikweta katika kampeni ya kuwania fainali hizo zitakazofanyika nchini Cameroon.