Mwameja, Pazi wampa neno kipa wa Yanga

Dar es Salaam. Kipa namba mbili wa Yanga, Metacha Mnata, amebaba matumaini ya timu hiyo katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Jicho la mashabiki wa soka linamuangalia Mnata kwa kuwa ndiye kipa atakayecheza mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika jijini Gaborone, Botswana.

Mchezo huo utaamua kama Yanga itasonga mbele au vinginevyo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mechi ya awali, Dar es Salaam.

Kocha Mwinyi Zahera hana namna nyingine za kumpanga Mnata kujaza nafasi ya kipa namba moja Mkenya Farouk Shikalo kutokuwa na leseni ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kipa huyo ameandaliwa kudaka na atasaidiwa na chipukizi Ramadhani Kabwili ambaye kwa sasa ni chaguo la pili kati ya makipa hao.

Tayari Mnata amecheza mechi mbili ngumu za kimataifa ikiwemo ile ya Taifa Stars katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) ambayo ilifungwa mabao 3-0 dhidi ya Algeria.

Kipa nguli wa zamani wa Simba, Idd Pazi alisema kitendo cha mchezaji huyo kucheza dhidi ya Rollers kitampa nafasi katika kikosi cha kwanza Yanga.

Pazi alisema amemuona Mnata katika mechi za Yanga ni kipa mwenye uwezo wa kuibeba timu na amewataka wachezaji na kocha kumuamini.

“Hii dhahabu kwa Mnata, akifanya kweli atakuwa amemuweka benchi Mkenya Farouk Shikalo, naamini hana hofu kwa kuwa tayari alicheza mechi ya kwanza,”alisema Pazi.

Pazi alisema ana matumaini Mnata akiandaliwa kisaikolojia anaweza kufanya maajabu na kubadili fikra za viongozi wa Yanga kusajili makipa wa nje.

“Mechi atakayodaka Mnata imebeba mambo mengi, kwanza kuivusha timu hiyo hatua nyingine, lakini pia kuondoa fikra za mabosi wake kuamini ana uwezo,”alisema Pazi.

Aliyekuwa ‘Tanzania One’, Mohammed Mwameja alisema hamtazami Mnata kuisaidia Yanga pekee, bali ataifanyia makubwa Taifa Stars.

Mwameja alimtaka kipa huyo kujiamini Jumamosi na awe anazungumza na mabeki wake bila kuwaogopa, kuwa makini na mipira ya krosi alizodai ndizo zinazotumiwa zaidi na Rollers.

“Township Rollers ni wazuri kwa mipira ya klosi, anatakiwa asiruhusu na awe anaongea na mabeki wake mara kwa mara, kubwa zaidi kocha amuongezee mbinu na awe anajiamini, ipo siku huyo kipa atafanya makubwa kwenye kikosi cha Stars,”alisema.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua, alimshauri Zahera kumjengea Mnata kujiamini ili kuona mchezo huo wa kawaida kama ilivyo mingine ya ndani.

“Mnata kwasasa asipewe vitu vingi, naamini kadri anavyocheza ndivyo anavyozidi kupata uzoefu, kocha na wachezaji wenzake wamuamini na kumpa nguvu kwasababu ndiye ameibeba Yanga,”alisema nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars.