Mwera mshindi wa medali ya dhahabu aliyestaafu riadha kwa utatanishi

Miongoni mwa wanariadha nyota waliotamba kwenye mbio za kati duniani, huwezi kuacha kumtaja Samwel Mwera, bingwa wa Afrika aliyestaafu mbio katika mazingira ya kutatanisha.

Mwera ndiye mwanariadha mwenye rekodi ya kustaafu mbio hapa nchi akiwa bado yuko katika kiwango bora, wengi hawakuamini kama mwanariadha huyo wa mbio za kati ametundika daluga.

Umbo la mwanariadha huyo, umri na rekodi yake vilitosha kuwaaminisha Watanzania kuwa atakuwa kwenye kiwango bora kwa muda mrefu na kuitangaza Tanzania katika mbio za kati duniani, lakini ilikuwa tofauti na matarajio ya wengi.

Nini kilimsibu Mwera

Akiwa kijana na bingwa wa medali ya Michezo ya Afrika ya mbio za mita 800 katika mashindano yaliyofanyika Abuja, Nigeria mwaka 2003, Mwera aliamua kutundika daluga.

“Nilipata maumivu ya miguu sikujua chanzo cha maumivu yale, ilitokea ghafla tu, wiki chache baada ya kushinda medali ya dhahabu ya Afrika,” anasema Mwera.

Anasema hakukimbia tena kwa kiwango chake kutokana na maumivu yale ambayo hakujua chanzo chake na hata kwenye Olimpiki ya 2004 kule Athens, Ugiriki japo alimaliza katika nafasi ya nne alikimbia kwa dakika 01:45:30 mbio za mita 800 lakini alikuwa na maumivu.

“Nilijaribu tiba mbalimbali bila mafanikio, nilipona baada ya kuamua kustaafu riadha kwa lazima baada ya miguu kunigomea kabisa nikiwa kwenye mbio za dunia, Osaka Japan.

Wakati ule nilikuwa bado mdogo kiumri, nilistaafu nikiwa katika kiwango bora sana, kila aliyenifahamu katika riadha alisikitishwa na uamuzi wangu ila sikuwa na namna miguu ilinigomea kabisa” anasema Mwera ambaye hadi anastaafu alikuwa na medali moja ya dhahabu na shaba mbili moja ikiwa ya mbio za dunia za vijana.

Rekodi

Tangu amestaafu zaidi ya miaka 11, rekodi ya nyota huyo wa zamani wa mbio za mita 800 haijawahi kuvunjwa nchini.

Mwera alistaafu akiwa na rekodi ya kukimbia kwa dakika 01:45 ikiwa ni sekunde nne tu nyuma ya nyota wa dunia raia wa Kenya David Rudisha ambaye ana rekodi ya kukimbia kwa dakika 01:41.

“Niliposhinda medali ya Afrika, nilikuwa na ndoto ya kushinda dhahabu ya Olimpiki na mbio za dunia, bahati mbaya ndoto yangu iliyeyuka kama barafu kutokana na maumivu ambayo hadi sasa sijui chanzo chake. Tangu Mwera (wa pili kushoto) amestaafu mwaka 2007, Tanzania haijapata mwanariadha nyota wa mbio za mita 800 ambaye ameweza kuvaa viatu vya nyota huyo kimataifa aliyekuwa pia akikimbia mbio za mita 1500.