Nigeria yaivulia kofia Burundi AFCON

Tuesday June 25 2019

 

Licha ya kuanza vyema fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), Kocha wa Nigeria, Gernot Rohr amesema Burundi si timu ya kuifanyia masihara katika michuano hiyo.

Kauli ya Rohr imekuja muda mfupi baada ya Nigeria ‘Super Eagles’ iliyokuwa ikipewa nafasi ya kuibuka na idadi kubwa ya mabao, kupata ushindi kiduchu wa bao 1-0 juzi usiku.

Kocha huyo alisema Nigeria ilishindwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 65, kwa kuwa Burundi ilicheza kwa nidhamu.

“Tulijua Burundi haikupoteza mchezo katika mechi za hatua ya kufuzu, hivyo tulitambua mechi itakuwa ngumu. Timu za aina hii zinatufahamu vizuri, zinajiandaa kucheza kwa nidhamu dhidi yetu,”alisema Rohr

Kocha huyo alidai katika mchezo huo, Burundi iliziba mianya ya kufunga mabao na haikushangaza kuambulia bao moja.

Burundi ilicheza kwa nidhamu hasa kipindi cha kwanza na kipa Daniel Akpeyi alifanya kazi ya ziada kuokoa kiki mara mbili za washambuliaji wa Burundi zilizoelekea kujaa wavuni.

Advertisement

Moja ya shambulizi kali iliyofanya Burundi ni Cedric Amissi alipoipenya ngome ya Nigeria, lakini Akpeyi aliokoa.

Burundi inayoshiriki michuano hiyo kama timu isiyopewa nafasi ya kufanya maajabu, ilikosa bao pale beki Frederic Nsabiyumva alipopiga mpira wa kichwa uliogonga mwamba.

Hata hivyo, kipindi cha pili Nigeria ilitumia uzoefu katika michuano ya kimataifa kwani dakika ya 77 ilipata bao hilo lililofungwa na mchezaji aliyetokea benchi Odion Ighalo.

Mshambuliaji wa FC Midtjylland, Paul Onuachu nusura afunge bao dakika ya 12 kama si uhodari wa kipa wa Burundi Jonathan Nahimana kuokoa mpira wake wa kichwa uliokuwa ukienda kujaa wavuni.

Burundi inayoshika nafasi ya 134 kwa viwango vya soka duniani, iliongozwa na nahodha wake anayecheza klabu ya Stoke City ya England Saido Berahino.

Advertisement