Nyoni, Domayo watoa neno

Dar es Salaam. Wakati wachezaji wa zamani wa Taifa Stars walioipa tiketi ya kucheza Fainali za Afrika Kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) wakitoa maoni tofauti, nyota wa timu hiyo wamesema watacheza kufa au kupona kupata matokeo mazuri dhidi ya Sudan.

Taifa Stars na Sudan zinavaana kesho katika mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika Cameroon, mwakani.

Akizungumza Dar es Salaama jana, Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliwataka wachezaji wa Taifa Stars kuwa na mtazamo wa kupata ushindi.

“Nakumbuka mwaka 2008 wachezaji tulikuwa na ushirikiano, tulipeana morali na tulihamasishana kwa kuwa tulikuwa ugenini tukicheza mechi ngumu yenye kuamua hatima ya Tanzania,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Simba. Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Henry Joseph alisema mchezo huo ni mgumu na wanacheza mbele ya mashabiki wa Sudan wenye uzoefu na mashindano ya kimataifa.

Henry anayechezea Mtibwa Sugar, alisema Taifa Stars inapaswa kucheza kwa kujiamini, nidhamu na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ambayo yatakuwa silaha ya kupata ushindi.

“Nakumbuka walikuwa wakitumulika na tochi, walitufanyia fitina sana, lakini hazikutuzuia kutimiza lengo letu. Zama zimebadilika kwa hiyo ni vyema wakajiandaa kukabiliana na changamoto ya aina yoyote ambayo inaweza kujitokeza,” alisema mchezaji huyo.

Wakati kina Mgosi wakitoa maoni hayo, Erasto Nyoni alisema morali ya timu ni kubwa na wamejiandaa kukabiliana na Sudan katika mazingira yoyote.

Frank Domayo alisema wamekubaliana kucheza kufa au kupona ili kupata matokeo mazuri dhidi ya Sudan na kila mmoja anatambua umuhimu wa mchezo huo.

Kwa upande wake, Ditram Nchimbi alisema kocha Etienne Ndayiragije amekuwa akiwataka kucheza kwa ari huku wakikumbuka kwamba ni wawakilishi wa Watanzania.

“Kuna joto kali, lakini haliwezi kuwa sababu ya kushusha kiwango chetu, tumejiandaa vizuri na mwalimu amekuwa pamoja nasi muda wote,” alisema Nchimbi.

Taifa Stars ilifungwa bao 1-0 na Sudan katika mchezo uliofanyika Septemba 22 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo ilifuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kuitoa Sudan kwa kuifunga jumla ya mabao 5-2. Taifa Stars ilishinda nyumbani mabao 3-1 mchezo wa kwanza kabla ya kuilaza Sudan ugenini 2-1.