Nyundo 5 kwa kocha mpya wa Simba SC

Dar es Salaam. Kocha Sven Ludwig Vandenbroeck ndiyo habari ya mjini hivi sasa kwenye kikosi cha Simba lakini ili kutetea ‘ugali’ wake Mbelgiji huyo atalazimika kukwepa nyundo tano nzito ambazo zilimuangusha mtangulizi wake, Patrick Aussems.

Vandenbroeck ambaye juzi Alhamisi kwa mara ya kwanza alishuhudia mazoezi ya Simba, atatakiwa kukwepa nyundo ya kwanza kwenye mechi za Kombe la Shirikisho (FA).

Msimu uliopita mtangulizi wake alishindwa kufika mbali baada ya kuruhusu kipigo katika hatua za awali dhidi ya timu ndogo ya Mashuja United, jambo ambalo liliwakera mashabiki wa Simba.

Vandenbroeck atakuwa na kibarua cha kuiongoza Simba kushinda mchezo wa awali dhidi ya AFC inayocheza Ligi Daraja la Kwanza, hicho kitakuwa kipimo chake cha kwanza tangu alipotua Simba Jumatano iliyopita.

Simba na Yanga

Mechi ya Januari 4 kati ya watani hao wa jadi itakuwa nyundo nzito zaidi kichwani kwa Vandenbroeck katika ajira yake hiyo mpya.

Mashabiki wa Simba hawatakubali kufungwa na watani zao katika mechi hiyo, kipindi ambacho Yanga imekuwa kwenye mtikisiko wa uchumi kwa miezi kadhaa huku baadhi ya wachezaji wake wa kigeni wakivunja mikataba kwa kutolipwa mishahara kwa miezi mitatu.

Licha ya mechi ya Simba na Yanga kutotabirika, lakini itakuwa ni pigo kwa Simba ambao wanaamini wana kikosi kupana kufungwa na Yanga yenye hali tete kiuchumi hivi sasa.

Nidhamu ya timu

Moja ya vitu ambavyo vilielezwa na muwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji (Mo Dewji) kuwa vilichangia kumuondoa Aussems ni nidhamu mbovu.

Katika mkutano mkuu wa Simba, Mo Dewji alisema baadhi ya wachezaji hawana nidhamu na kusisitiza kuwa nidhamu ni moja ya vitu vilivyochangia kuachana na Aussems.

Mrithi wake atakuwa na jukumu la kuhakikisha anaimarisha nidhamu katika kikosi hicho, jambo ambalo huenda likapokewa kwa mtazamo hasi au chanya na wachezaji ambao wanatuhumiwa na Mo Dewji kuwa watovu wa nidhamu.

Soka la kuvutia

Katika vitu ambavyo Mo Dewji alieleza vinamkera ni kiwango cha timu. Alisema licha ya timu hiyo kuongoza ligi, haridhishwi na kiwango wanachokionyesha uwanjani.

Huo utakuwa ni mtihani mwingine kwa Vandenbroeck kuhakikisha kikosi cha Simba kitacheza soka la kuvutia kama ambavyo Wana Simba wanatamani.

Ingawa Mo Dewji amewahakikishia wanachama wa Simba kwenye mkutano mkuu kwamba, mrithi wa Aussems ni kocha mwenye kiwango bora ambaye ana sifa za kuinoa Simba.

Kutetea ubingwa

Katika vitu ambavyo Simba hawatapenda kuvikosa msimu huu ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ambao imeushikilia kwa misimu miwili mfululizo.

Huu ni mtihani mwingine kwa kocha Vandenbroeck ambaye ameanza kukinoa kikosi hicho kikiwa kinaongoza ligi.

Mbali na ubingwa, kocha huyo atakuwa na kibarua kingine cha kuhakiksha Simba inafuzu na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, licha ya msimu huu kutolewa katika hatua za awali. Mtangulizi wake aliifikisha katika robo fainali msimu uliopita.

Iddi Pazi, Mogella walonga

Kipa wa zamani wa Simba, Iddi Pazi alisema kilichopo sasa ni kocha huyo kupewa muda ili afanye kazi.

“Kikubwa tumpe ushirikiano, yeye binafsi hawezi kutufufikisha katika mafanikio ambayo tunatamani,” alisema Pazi.